WACHANGIA WAHANGA WA MELI


viongozi wamathehebu mbalimbali wakiwa kwenye uchangiaji wa fedha za wahanga wa meli


UMOJA wa madhehebu yote ya kidini wilaya ya Arusha imefanikiwa kuchangisha kiasi cha shilingi milioni 3.6 kwaajili ya kusaidia waathirika wa tukio la ajali ya meli ya MV Spice Island iliyotokea hivi karibu visiwani Zanzibar .

Akizungumza kuhusiana na michango hiyo mmoja wa viongozi wa waumini hao Ghullamhussein.R.Mukhtar alisema fedha hizo ziatawakilishwa moja kwa moja kwa makamu wa pili wa Rais Balozi Seif Ally Idd kwaajili ya kuwafikia waathirika wa janga hilo.

Alisema fedha hizo zilipatikana kupitia michango iliyofanyika kupitia dua maalumu iliyofanywa na viongozi wa madhehebu hayo na viongozi wa kiserikali kwaajili ya kuwaombea marehemu na waathirika wa tukio hilo .

Aidha alisema katika kuhakikisha fedha hizo zinafika kamilifu na kutumika kwa lengo lililokusudiwa wameweka mikakati mahususi ya ya kufikisha fedha hizo ikiwa ni pamoja na kutuma fedha hizo katika akaunti maalumu na sio kupitia kwa mtu binafsi.

Alitaja jina la akaunti inayotumika kutumia fedha hizo kuwa ni ile yenye jina Zanzibar Disaster Fund yenye namba 051103000013 na kuwasihi wale wote wenye kutaka kutoa michango yao kutuma kwenye akaunti hiyo hapo juu.

Katika michango hiyo umoja wa makalasinga Arusha kupitia kwa mwenyekiti wao walichangia kiasi cha shuilingi milioni 1,kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania KKKT kupitia kwa askofu wake Thomas Laizer liliweza kuchangia shilingi milioni 1 pia.

Wengine waliochangia ni jeshi la polisi mkoa wa Arusha kupitia kwa mkuu wake wa upelelezi RCO Leonard Paul aliyetoa shilingi 200,000,Taasisi ya Hindu mkoani Arusha nayo ilichangia shilingi 500,000,Taasisi ya Suni Arusha nayo ilichangia shilingi 600,000 huku baraza la waislamu mkoa wa Arusha Bakwata likichangia shilingi 500,000 wakati jumuiya ya Khoja Shia Ithnaasheria ya shirikisho la Afrika walishachangia kiasi cha shilingi milioni 30 kwaajili ya janga hilo.

Hata hivyo Ghullam alisifu ushirikiano ulioonyeshwa na madhehebu hayo katika kufanikisha dua na michango hiyo na kusisitiza umoja huo ulioonyeshwa uendelezwe katika shida na hata raha.

Pia aliwatakia afya njema wale waliookoka katika ajali hiyo waliopo mahospitalini na kuwatakia rehma za mwenyezi Mungu marehemu wote wa janga hilo .

Katika ajali hiyo iliyotokea usiku wa jumamosi iliyopita katika eneo la Nungwi mjini Zanzibar ilisababisha vifo vya watu 204 na kujeruhi wengine 500 baada ya meli hiyo kuzama kutokana na kuzidiwa mzigo wa abiria na mizigo.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post