WATU WAWILI WAFARIKI DUNIA KATIKA MATUKIO MAWILI TOFAUTI

WATU wawili wamefariki dunia kwa ajali katika matukio mawili tofauti mjini Arusha.


Kaimu Kamanda wa polisi mkoani hapa, Akili Mpwapwa alisema kuwa tukio la kwanza limetokea septemba 19 mwaka huu majira ya saa 11;30 jioni katika eneo la Malulo King’ori katika barabara ya Arusha –Moshi .


Alisema kuwa , gari aina ya Nissan Lori yenye namba za usajili SU 37442 mali ya mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro ikiendeshwa dereva aliyetambulika kwa jina la Monday Nanka (38) mkazi wa Ngorongoro lilimgonga mwendesha baiskeli aitwaye Anold Ainea (14) na kufariki dunia papo hapo.


Mpwapwa alisema kuwa, marehemu alikuwa ni mwanafunzi wa shule ya Malula iliyopo eneo la King’ori wilayani Arumneru na kwamba alikuwa akitoka shuleni kuelekea nyumbani.


Alisema kuwa, dereva wa gari hilo anashikiliwa na polisi na pindi uchunguzi utakapokamilika atafikishwa mahakamani kujibu shitaka hilo, huku mwili wa marehemu ukihifadhiwa katika hospitali ya mkoa ya Mount Meru.


Wakati huo huo, mtoto mwenye umri wa miaka (2) aliyetambulika kwa jina la Benjamini Samweli mkazi wa Sinoni Daraja mbili amefariki dunia baada ya kugonjwa na gari wakati akicheza nyumbani kwake.


Kaimu Mpwapwa alisema kuwa, tukio hilo limetokea septemba 18 mwaka huu majira ya saa 7;00 mchana katika eneo la Sinoni daraja mbili ambapo gari aina ya Nissan Min Bus lenye namba za usajili T 264 likiendeshwa na dereva ambaye hakuweza kufahamika jina lake kutokana na kukimbia mara baada ya ajali hiyo.


Mpwapwa alifafanua zaidi kuwa, siku ya tukio mtoto huyo alikuwa akicheza nyumbani kwake, ambapo dereva huyo alipita katika barabara iliyopo ndani ya makazi ya watu , na kukuta mtoto huyo akicheza ndipo alipomgonga na kufa hapo hapo.


Aidha mara baada ya ajali hiyo dereva huyo aliacha gari hilo eneo la tukio na kukimbia kusikojulikana ambapo askari wa usalama barabarani waliweza kufika eneo la tukio na kulichukua gari hilo ambalo limehifadhiwa katika kituo cha polisi.


Mpwapwa alisema kuwa , dereva wa gari hilo anasakwa na jeshi la polisi kuhusiana na tukio hilo,huku mwili wa marehemu ukiwa umehifadhiwa katika hospitali ya mkoa ya Mount Meru.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post