Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha
Kamishna Msaidizi wa Polisi Liberatus Sabas akiwaonyesha waandishi wa
habari madawa ya kulevya aina ya bangi ambayo yalikuwa kwenye magunia 97
yaliyokamatwa na askari wa jeshi hilo katika eneo la Usa river wilayani
Arumeru
Askari wa jeshi la polisi wakiwa
wanashusha magunia ya madawa ya kulevya aina ya bangi mara baada ya
kukamatwa eneo la Usa River wilayani Arumeru yakiwa yanasafirishwa
kwenye gari aina ya Fuso lenye namba za usajili T.282 AAJ kuelekea Moshi
Jeshi la Polisi mkoani hapa
limemkamata mtu mmoja akiwa na magunia 97 ya madawa ya kulevya aina ya
bangi ambayo yalikuwa yanasafirishwa toka mkoani hapa kuelekea Moshi.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha
Kamishna Msaidizi wa Polisi Liberatus Sabas amesema kwamba, tukio hilo
lilitokea muda wa saa 10:00 alfajiri eneo la Usa River wilayani Arumeru.
Alisema mafanikio hayo
yametokana na ushirikiano mzuri kati ya jeshi hilo na wananchi ambapo
taarifa za tukio hilo zilitolewa na raia wema ambapo askari wa jeshi
hilo waliweka mtego eneo hilo na kufanikiwa kulikamata gari aina ya Fuso
lenye namba za usajili T. 282 AAJ.
Kamanda Sabas aliongeza kwa
kusema kwamba, ndani ya bodi ya gari hilo kulikuwa na mboga aina ya
kabeji iliyosambazwa vizuri huku chini ya mboga hiyo kukiwa na madawa
hayo yaliyokuwa kwenye magunia huku yakivingirishwa kwenye mifuko ya
“plastiki” kwa ndani.
Alisema katika gari hilo
kulikuwa na watu watatu na mara baada ya askari hao kulisimamisha dereva
pamoja na msaidizi wake walifanikiwa kukimbia huku mtu mmoja
aliyejulikana kwa jina la Praygod Marick (22) Mkazi wa Dar esalaam
akikamatwa.
Jeshi la polisi Mkoani hapa
linaendelea kumhoji mtuhumiwa huyo huku watuhumiwa wengine wakiendelea
kutafutwa. Kwa mara nyingine tena Kamanda huyo aliendelea kuwashukuru
wananchi wa Mkoa huu kutokana na ushirikiano wao mkubwa wanaoutoa kwa
jeshi hilo na kuendelea kuwasisitizia kuimarisha mahusiano na jeshi
hilo.
Kwa muda wa kipindi cha mwezi
mmoja toka januari 07, 2013 mpaka hivi leo jeshi hilo limeshakamata
madawa ya kulevya aina ya mirungi magunia 372 katika magari mawili
tofauti na pia limeshakamata jumla ya magunia 117 ya madawa ya kulevya
aina ya bangi ambapo mwanzoni mwa wiki hii jumla ya magunia 20
yalikamatwa yakiwa yanasafirishwa kwa kutumia wanyama aina ya Punda
maeneo ya Losoiti wilayani Longido.