BREAKING NEWS

Thursday, February 7, 2013

MKUU WA WILAYA AONYA WANAOTUMIA JINA LAKE KUTAPELI

Mkuu wa wilaya ya Hai,Novatus Makunga amewata wananchi wilayani humo na wilaya za jirani kuwa makini na matapeli wanaotumia nafasi yake  ya ukuu wa wilaya kutangaza kwamba kuna nafasi za ajira katika kampuni moja ya madini inayochimba katika migodi ya Tanzanite iliyopo Mererani wilayani Simanjiro mkoani Manyara.

Mkuu huyo wa wilaya,Makunga ametoa ufafanuzi huo wakati anazungumza na waandishi wa habari ofisini kwake katika mji wa Bomang'ombe uliopo wilayani Hai.

Amesema kuwa siyo kweli kwamba kampuni ya afrika ya kusini inayochimba madini ya Tanzanite huko Mererani ya Tanzanite one inatoa ajira za kazi kupitia ofisi ya mkuu wa wilaya ya Hai.

Makunga ameeleza kuwa amefikia hatua hiyo baada ya zaidi ya wiki mbili makundi ya vijana na wazee pamoja na wastaafu kutoka katika vyombo vya ulinzi kufurika ofisini kwake kutafuta kazi za kampuni hiyo.

Ametaja mbali ya vijana kundi hilo la watafuta ajira linawahudisha askari wastaafu wa jeshi la polisi pamoja na majeshi mengine wanaotafuta nafasi za maofisa wa usalama katika kampuni hiyo.

Makunga ameeleza watu hao mbali ya kutoka katika wilaya ya Hai pia wanatoka katika miji ya Arusha na Moshi.

Ameeleza kuwa taarifa hizo ni za ajabu kwa kuwa migodi ya kampuni ya Tanzanite One haipo wilayani Hai bali ipo katika wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.

Akifafanua,ameeleza kuwa ulaghai huo umefanywa na baadhi ya watu wanaojitafutia umaarufu katika wilaya ya Hai wa kuonekana wapo karibu zaidi na yeye kama mkuu wa wilaya.

Ameeleza kuwa amejaribu kutafuta chanzo cha taarifa hizo na kubaini kwamba mbali ya kundi hilo la watafuta umaarufu pia kuna kundi lilijipanga kutaka kuwatapeli fedha vijana kwa kuwahakikishia kupata ajira katika kampuni hiyo ya Tanzanite one.

Makunga ameeleza cha ajabu wimbi hilo limewakumba mpaka viongozi ma wakuu wa taasisi mbalimbali za umma na binafsi wilayani Hai ambao wamekuwa wakimpigia simu na wengine kufika ofisini kwake.

Ameeleza kuwa alilazimika kuupigia simu uongozi wa  Tanzanite kupitia meneja wa raslimali watu ambaye naye alistushwa na habari hizo na kueleza wazi kuwa kampuni hiyo haijatangaza nafasi yoyote ya kazi.

Amesema kuwa aliwashauri viongozi wa Tanzanite One kubandika matangazo ya kutokuwepo kwa nafasi za kazi katika maeneo yote ya miji kama ilivofanya katika eneo la migodi yake huko mererani.

Kutokana na kampuni hiyo kuwa ya pekee inayotumia teknolojia ya kisasa katika migodi ya Mererani na hivyo kuwa na uhakika wa madini watu wengi katika mikoa ya Kilimanjaro na Arusha hasa vijana wamekuwa wakiamini kwa kupata kazi hao ni moja ya njia ya kuwa matajiri.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates