KATA ya Endiamtu iliyopo Mji mdogo wa Mirerani
Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara,imefanikiwa kukusanya kiasi cha sh21.658
milioni za mfuko wa elimu kwa mwaka jana ambazo zimetumika kuinua elimu katika
kata hiyo.
Akizungumza juzi kwenye kikao cha maendeleo
cha kata hiyo (WDC) Ofisa mtendaji wa kata hiyo,Edmund Tibiita alisema fedha hizo zilichangwa na wananchi
mbalimbali wa vitongoji vinne vinavyounda kata hiyo.
Tibiita alisema kitongoji cha Kazamoyo
walichanga sh8.3 milioni,Zaire walichanga sh2.7 milioni,Kairo walichanga sh750,000,kitongoji
cha Sekondari walichanga sh2 milioni na kitongoji cha Kilimahewa walikusanya sh2
milioni.
Alisema askari polisi wakiongozwa na mkuu wa
kituo cha polisi Mirerani ASP Ally Mkalipa,walitoa sh310,000 Diwani wa kata ya
Endiamtu,Lucas Zacharia alijitolea sh3 milioni na wamiliki wa magari ya DCM
walijitolea sh360,000.
“Wengine waliotuchangia ni marafiki wa Diwani
wetu Lucas waliojitolea sh2 milioni,wafanyabiashara wa maduka sh830,000 na
vifaa vilivyobambuliwa vina thamani ya sh375,000.” alisema Tibiita.
Naye,Diwani wa kata ya Endiamtu Lucas
Zacharia,aliwataka wazazi na walezi wa kata hiyo kutoa kipaumbele na kuzingatia
kuwapatia watoto wao elimu kwani kwa dunia ya sasa bila kuwa na elimu Taifa
litakuwa gizani.
“Elimu iwe ndiyo ajenda yetu ya kwanza kwa
sisi kata ya Endiamtu hivyo tujitahidi kwa kadiri ya uwezo wetu katika
kuhakikisha kuwa watoto wetu wanapata elimu bora na iliyo katika mazingira
mazuri,” alisema Zacharia.
Pia,alisema hivi sasa wanatakiwa kuweka nguvu
moja kwenye ujenzi wa madarasa ya shule mpya ya msingi Zaire na Endiamtu,kwani
shule za msingi Mirerani na Jitegemee hazina maeneo ya kujengewa madarasa
mapya.
Aliwataka wajumbe wa kamati ya maendeleo ya
kata hiyo (WDC) wajitolee kwa moyo mmoja,katika kuhakikisha kuwa wanawatumikia ipasavyo
wananchi waliowachagua kwani huu siyo wakati wa kufanya siasa.