Ticker

6/recent/ticker-posts

BITEKO AUNGA MKONO AGIZO LA WAZIRI MKUU KWA VITENDO, ACHANGIA MABATI 100 KUPAUA SHULE YA SEKONDARI AZIMIO


Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita ambaye ni Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko akihutubia mamia ya wananchi katika Kijiji cha Kilimahewa kilichopo katika kata ya Bulangwa wakati wa ziara za kijimbo hivi karibuni. 
Baadhi ya wananchi katika Kijiji cha Kilimahewa kilichopo katika kata ya Bulangwa wakifatilia hotuba ya Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita ambaye ni Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko wakati wa ziara za kijimbo hivi karibuni.

Na Mathias Canal, Bukombe-Geita

Mbunge wa Jimbo la Bukombe Mkoani Geita ambaye ni Naibu Waziri wa Madini Mhe Doto Mashaka Biteko ameendelea kutekeleza agizo la Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa alilolitoa 2 Aprili 2018 wakati wa dhifa ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2018 katika uwanja wa Magogo mkoani Geita Katika sherehe hizo zilizonakshiwa na Kaulimbiu ya mbio za mwenge kwa mwaka huu ambayo ni ‘Elimu ni ufunguo wa maisha, wekeza sasa kwa maendeleo ya Taifa letu.’

Waziri Mkuu aliwagiza viongozi wa mikoa ya Tabora, Geita, Mtwara na Shinyanga ambayo inaongoza kwa utoro wa wanafunzi kwa shule za msingi na kwa sekondari wahamasishe umuhimu wa elimu na mahudhurio endelevu shuleni kwani miongoni mwa sababu zinazopelekea wanafunzi kutoelimika ipasavyo ni pamoja na utoro shuleni.

Kupitia agizo hilo Mhe Biteko amechangia mabati 100 geji 28 yenye thamani ya Sh 2.6 milioni kwa ajili ya ukamilishaji wa kupaua vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari Azimio Wilayani Bukombe ikiwa ni sehemu ya hamasa kwa wanafunzi kuwa na maeneo bora ya kusomea.

Mara baada ya uzinduzi wa Mwenge huo wa Uhuru 2 Aprili 2018 kabla ya kuelekea Mjini Dodoma kwa ajili ya shughuli za Bunge zilizoanza 3 Aprili 2018 Mhe Doto Biteko alizuru Kijiji cha Nampalahala kilichopo Kata ya Busonzo na kujionea jinsi ujenzi wa maabara unavyoendelea ambapo pia alichangia matofali 10,000  kwa ajili ya ukamilishaji Wa vyumba vya maabara ili kurahisisha uanzishaji wa shule ya sekondari wa Kata ya Busonzo wilayani Bukombe.

Akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza juzi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Kilimahewa kilichopo katika kata ya Bulangwa, Mhe Biteko alisema kuwa Serikali ya awamu ya tano inyoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli, imedhamiria kuboresha elimu katika ngazi zote nchini, kuanzia Elimu ya Awali hadi Elimu ya Juu hivyo wananchi wanapaswa kuitumia fursa hiyo kwa maendeleo ya wilaya hiyo na Taifa kwa ujumla.

Alisisitiza kuwa serikali imeweka mkakati wa kutoa elimu bure kwa wanafunzi wote nchini kuanzia ngazi ya msingi hadi sekondari hivyo jukumu la wazazi ni kuwapeleka watoto shule ili kunufaika na matunda ya serikali katika utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaja 2015-2020.

Aliongeza kuwa wananchi wanapaswa kukiunga mkono Chama Cha Mapinduzi kwani ndicho chama pekee nchini kinachoshughulika na matatizo ya wananchi ikiwemo kuboresha shughuli mbalimbali za maendeleo katika kuboresha elimu, afya, miundombinu na huduma zingine zikiwemo upatikanaji wa maji.

Post a Comment

0 Comments