
Mradi wa maji wa Ngaramtoni na moja ya miradi wa maji ya vijiji
kumi umekamilika na unategemea kutumia teknolojia mpya ya 'eWaterpay' ya
kulipia maji kabla ya kutumia.
Hayo yamethibitishwa na Mkurugenzi Mtendaji, halmashauri ya Arusha,
Dkt. Wilson Mahera, wakati akifungua mafunzo ya siku nne yanayohusisha
wafanyakazi na wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Maji Ngaramtoni (NGAUWSA),
kwenye Ukumbi wa mikutano wa Golden Rose.
Mkurugenzi Mahera amesema kuwa mradio huo wenye thamani ya shilingi
milioni mia 7.9, unaotegemewa kukabidhiwa mapema wiki ijayo na tayari
vituo 21 vya kuchotea maji vimeanza kutoa maji kwa majaribio na vyote
vitafungwa mfumo wa 'eWaterpay' wa kulipia maji kabla ya kutmia.
Hata hivyo Dkt. Mahera amefafanua kuwa, mfumo huo unafanyika kwa
majaribio, baada ya kuona mafanikio ya mfumo huo, waliyoyapa wananchi wa
mkoa wa jirani wa Manyara kwenye halmashauri ya Babati.
Mkurugenzi Mahera, amethibitisha kuwa, mfumo huo unauwezo wa
kudhibiti mapato pamoja na kudhibiti upotevu wa rasilimali maji,
unaokwenda sambamba na utunzaji wa rasilimali maji hasa kwa kukizingatia
kuna changamoto ya upatikanaji wa maji,kwenye vyanzo vya maji.
"Tunatarajia teknolojia ya 'eWaterpay' kuboresha utaratibu mzima wa
utoaji huduma ya maji pamoja na upatikanaji wa huduma hiyo kwa wananchi"
amesema Mkurugenzi.
Aidha Dkt. Mahera amewataka watumishi na wajumbe wa Bodi ya Maji -
NGAUWSA kutumia mafunzo hayo, kuongeza kiasi cha upatikanaji wa huduma
za maji ndani ya maeneo yote ya Mamlaka ya Mji Mdogo Ngaramtoni.
Naye Mratibu wa shirika la eWater, Deogratius Nyusso, amethibitisha
kuwa, teknolojia ya 'eWaterpay' inarahisisha upatikanaji wa huduma ya
maji kwa watumiaji wa maji na kwa watoa huduma ya maji pia, na inauwezo
wa kutatua changamoto za miundo mbinu ya maji kwa haraka zaidi,kwa kuwa
mfumo unaruhusu kuona changamoto hizo ukiwa ofisini bila kufika eneo
husika.
"Teknolojia hii inamrahisishia mtumia maji kudhibiti matumizi yake
binafsi ya maji, kwa kulipia maji aliyoyatumia, pamoja na kuirahisishia
NGAUWSA kudhibiti ukusanyaji wa mapato, kufahamu endapo kuna uharibifu
wa miundombinu ya bomba, bila kufika eneo la tukio na kuweza kutengeneza
kwa wakati" amethibitisha Nyusso.
Nyusso ameongeza kuwa, lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo
watumishi hao kwenye maeneo ya ukusanyaji mapato kwa uwazi na uhakika,
kupitia teknolojia rahisi ya kutumia simu sambamba na utatuzi wa
changamoto za mifumo ya maji.
Naye Meneja wa NGAUWSA, Clayson Kimaro, ameonyesha namna matumizi ya
teknolojia hiyo, yatakavyorahisiha upatikanaji wa huduma za maji kwa
wananchi pamoja na uwezekano wa kuongezeka kwa upatikanaji wa huduma
hiyo katika eneo linalohudumiwa na NGAUWSA.
Hata hivyo, teknolojia hiyo ya 'eWaterpay' itatumika zaidi kwenye
mradi wa maji wa maji vijiji vitano, unaofadhiliwa Idara ya maendeleo ya
nchini Uingereza 'DFID' na kutekelezwa na shirika la WaterAid Tanzania,
unaotegemea kukamilika mwishonj mwa mwezi Septemba 2018 na unategemea
kuhudumia watu elfu hamsini.