
Halmashauri ya Wilaya ya Longido imepewa siku 7 kuhakikisha imejibu
hoja zote zilizotolewa na mkaguzi wa nje (CAG) kwa mwaka fedha kuanzia
2015 hadi 2017.
Akitoa agizo hilo mkuu wa mkoa wa Arusha Mrisho Gambo, amesema
halmashauri kupata hati ya mashaka kwa hoja zinazojibika na
zinazojirudia kila mwaka ni uzembe wa baadhi ya watumishi wa halmashauri
hiyo.
“Watumishi bado wapo wachache wanaofanya kazi kwa mazoea bila ya kufuata sheria na taratibu za kiutumishi”.
Ameuwagiza uongozi wa halmashauri ya Longido kutoa barua za onyo kwa
watumishi wote waliotajwa kwenye taarifa ya mkaguzi wa nje ili iwe
fundisho kwa watumishi wote umma.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha Richard Kwitega,amesema ifike wakati
sasa viongozi kutoonea huruma mtumishi yoyote anaebainika ana makosa,
kwani hoja nyingi katika halmashuri hiyo zimekuwa zikijirudiarudia kila
mwaka.
Amesema hatua madhubuti ni lazima sasa zichukuliwe ili kudhibiti tabia hii ya mazoea ya hoja kujirudiarudia kila mala.
Akisisitiza zaidi mkuu wa wilaya ya Longido Daniel Chongolo amesema
kazi ya viongozi ni kusimamia sheria na taratibu za kazi,hivyo
ataendelea kusimamia sheria za utumishi wa umma katika halmshauri yake
kwani mpaka sasa hali imeanza kubadilika kwa watumishi kuwa na nidhani.
Aidha, amesema halmshauri ipo tayari kutekeleza maagizo yote
yaliyotolewa na mkuu wa mkoa na kuhakikisha halmashauri yake haitapata
tena hati ya mashaka kwa miaka inayokuja.
Gambo yupo katika ziara ya siku 3 wilayani Longido ambapo atatembelea
miradi mbalimbali ya maendeleo iliyofanywa katika wilaya hiyo.