
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mrisho Gambo amesema wananchi wa kata ya
Kimokouwa na Namanga kwa ujumla hawana haja yakupata matibabu tena
kutoka nchi jirani ya Kenya.
Aliyasema hayo alipokagua ujenzi wa kituo cha afya cha Eworendeke katika kata ya Kimokouwa wilayani Longido.
Gambo amesema kwa mda mrefu sana wananchi wa Namanga kwa ujumla
walikuwa wanapata hadha yakufuata huduma ya matibabu Longido mjini au
nchi jirani ya Kenya na hivyo kufanya wagonjwa wengi kutembea umbali
mrefu.
Amesema kituo hicho cha afya kimepata mgao wa shilingi milioni 700
kutoka serikalini na wananchi wanachangia nguvu kazi katika kukijenga na
mpaka sasa kiasi cha milioni 400 ndio kimeshatumika na ujenzi
unaendelea.
Gambo amesema mbali na serikali kutoa kiasi hicho cha fedha bado
bajeti ya ununuzi wa madawa umeongezwa kutoka bilioni 31 hadi bilioni
269 kwa mwaka huu wa fedha, na hii itasaidia huduma ya madawa kupatikana
kiurahisi katika kila kituo cha afya na hospitali zote nchini.
Kituo cha afya cha Eworendeke kinatarajia kukamilika Agosti 2018 na
huduma zote zitapatikana zikiwemo huduma za upasuaji na x-ray, hivyo
itarahisisha matibabu kwa wananchi wote wa Namanga.
Mkuu wa Wilaya ya Longido Daniel Chongolo,amesema asilimia 27 ya
wajawazito walikuwa wanajifungulia katika vituo vya afya kwa wilaya
nzima na idadi imeongezeka kufikia asilimia 35.
Chongolo amesema ongezeko hili litasaidia kupunguza vifo vya mama na mtoto katika wilaya yake.
Mgaga mkuu wa Mkoa Dokta Vivian Wonanji,amesema serikali imeshatenga
kiasi cha fedha cha milioni 200 kwa ajili ya manunuzi ya vifaa kwa vituo
vyote vya afya na hospitali kwa mkoa mzima na anaendelea na zoezi la
kuongeza watumishi katika sekta ya afya.
Amesema agizo la serikali ni kuhakikisha vituo vyote vya afya
vinakuwa na huduma ya x-ray, hivyo katika kituo hicho wanajenga chumba
maalumu kitakachotoa huduma hiyo kwa wananchi wote wa Namanga.
Akitoa shukurani zake za dhati kwa serikali bwana Hassan Hamis ambae
ni mkazi wa Namanga amesema kweli kituo hicho cha afya kitasadia
kuondokana na hadha waliyokuwa wanaipata kufuata matibabu kwa umbali
mrefu, na pia itapunguza vifo vilivyokuwa vinatokana na umbali huo.
Gambo anaendelea na ziara yake katika wilaya ya Longido ambapo
ametembelea kituo kingine cha afya cha Engarenaibor kilichogharimu
kiasi cha milioni 200, pia ameshiriki ujenzi wa kituo cha afya cha kata
ya Ketumbeine.