Wachungaji watatu wamenusurika kipigo kutoka kwa wananchi, baada ya
kushindwa kumfufua marehemu katika Kijiji cha Sitalike Tarafa ya Nsimbo
Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi.
Wachungaji hao walifika kijijini hapo wakidai kuwa wanao
uwezo wa kumfufua marehemu mwanakijiji mwenzao aliyefariki dunia hivi
karibuni na kuzikwa kwenye makaburi ya Kijiji hicho.
Akisimulia tukio hilo, mwenyekiti wa kijiji hicho,
Christopher Angelo, alisema kuwa tukio hilo lililovuta hisia za watu
wengi lilitokea Mei 7, majira ya saa 4 za asubuhi kijijini hapo.
Alisema kuwa wachungaji hao ambao walikuwa watatu walifika
kwenye ofisi ya Kijiji na kujitambulisha kuwa wao ni wachungaji wanatoka
katika Kijiji cha Nsimbo na watakuwapo kijijini hapo wakiwa wameitwa na
ndugu wa marehemu, Raymond Mirambo aliyefariki dunia siku moja na
kuzikwa kijijini hapo.
Alisema wachungaji hao walifika kijijini hapo wakidai kuwa
wanataka kufanya maajabu ambayo ni ya kihistoria nchini ya kufanya
maombi mfululizo na kumfufua marehemu Raymond.
Mwenyekiti huyo alisema kutokana na kujitambulisha kwa
wachungaji hao kwenye ofisi ya kijiji, uongozi wa kijiji uliwaruhusu
wachungaji hao kufanya maombi hayo ya kumfufua marehemu huyo.
Alisema baada ya kuruhusiwa na uongozi wa kijiji walielekea
nyumbani kwa marehemu na kuwakuta ndugu wakiwa wanawasubiri kwa ajili
ya maombi hayo ya kumfufua ndugu yao.
Alisema maombi hayo yaliendelea kwa muda wa siku saba usiku
na mchana pasipo kuwa na mafanikio yoyote, hali ambayo iliwafanya ndugu
wa marehemu washikwe na hasira.
“Wananchi, ndugu na jamaa walikasirika kutokana na kuona
kuwa wachungaji hao wanawatapeli na kwa sababu waliwasababishia kuingia
gharama kubwa ya kulisha watu waliokuwa wakishiriki maombi hayo,”
alisema.
Kwa mujibu wa Angelo, baada ya kuona hafufuki, ndugu
wakiongozwa na mama mzazi wa marehemu waliamua kwenda kutoa taarifa
ofisi ya kijiji, ili kuepusha vurugu ambazo zilitaka kutokea.
Alisema watu walioonekana kuwa na hasira kwa kutoona
muujiza wa kumfufuka marehemu walitaka kuwapiga wachungaji hao kwa
kuwapotezea muda na kuwatapeli.
Mwenyekiti huyo alisema viongozi wa Kijiji baada ya kufika
kwenye eneo hilo walikuta ndugu wa marehemu wakiwa wanafoka kwa hasira
huku wakiwa wanawatuhumu wachungaji hao kuwa ni matapeli.
“Sisi uongozi wa Kijiji tulikuta vurugu na wananchi
walikuwa wanataka kuwapiga wachungaji hao, tulichofanya kuepusha shari
ni kuwaondoa wachungaji hao eneo hilo na kwa kweli walitii agizo hilo na
kuondoka zao,” alisema Angelo.