
Wauguzi halmashauri ya Arusha, wameungana na wauguzi wenzao
duniani, kuadhimisha siku ya Wauguzi duniani huku halmashauri yao ikiwa
na mafanikio makubwa katika uboreshaji wa miundombinu ya afya katika
vituo vyake vya kutolea huduma za afya katika maeneo ya pembezoni.
Kama inavyofahamika, mazingira bora ya kazi ikiwemo ubora wa
miundombinu na uwepo wa vifaa tiba katika maeneo ya kutolea huduma za
afya, humuwezesha muuguzi kufanya kazi yake kwa kujiaamini na kwa weledi
zaidi.
Hata hivyo wauguzi hao wamekiri kwa njia ya wimbo kwa kuthibitisha
kuwa, wao hujisikia wanyonge pindi mgonjwa anapofika hospitali kupata
huduma na huduma hiyo kukosekana katika eneo hilo la kazi.
Akihutubia wakati wa maadhimisho hayo, mgeni rasmi na Mkurugenzi
Mtendaji wa halmashauri ya Arusha Dkt. Wilson Mahera, amekiri kuwa,
halmashauri ya Arusha inaadhimisha siku ya wauguzi duniani huku ikiwa na
mafanikio makubwa katika kuboresha miundombinu ya vituo vya afya kwenye
maeneo ya pembezoni ya kata za Nduruma, Mlangarini na Bwawani, kata
ambazo kwa muda mrefu, wananchi wake wamekuwa wakiteseka kutafuta huduma
hizo, kwa umbali wa zaidi ya kilomita 30.
Mkurugenzo huyo, ameongeza kuwa, licha ya uboreshaji wa vituo hivyo
vya afya kuwanufaisha wananchi wa maeneo hayo lakini pia unawarahisishia
wauguzi kutoa huduma kwa wagonjwa na wateja wao kwa ufanisi na weledi.
Amefafanua kuwa jumla ya vituo viwili vya afya, vimeboreshwa na kuwa
na sifa ya nyota tano katika kata ya Nduruma na Mlangarini kwa
kukarabati na kuongeza majengo, kwa ajili ya upanuzi wa utoaji wa huduma
zote muhimu.
Amevitaja vituo hivyo ni pamoja na kituo cha afya Nduruma
kilichogharimu shilingi milioni 500 na kituo cha afya Manyire,
kinachomaliziwa kwa ufadhili wa Ubalozi wa Japan nchini Tanzania kwa
gharama ya shilingi milioni 190.
Aidha Dkt. Maera ameendelea kusema kuwa, vituo hivyo vyenye hadhi ya
nyota tano, vitatoa huduma za wagonjwa wa nje na wakulazwa, huduma za
uzazi, kliniki ya mama na mtoto, upasuaji na huduma za maabara.
Amewahakikikishia wauguzi na wananchi wa maeneo hayo kuwa, tayari
serikali imeshaagiza vifaa tiba kwa ajili ya kituo cha afya Nduruma
vyenye thamani ya shilingi milioni 220 kutoka Bohari kuu ya Dawa 'MSD'
na muda mfupi vitawasili na kuanza kuwapatia huduma.
Licha ya kuwepo na vituo hivyo viwili vya afya kwa maeneo ya
pembezoni, Mkurugenzi huyo ameweka wazi kuwa, kwa sasa halmashauri
imeanza kutoa huduma ya Mkoba 'mobile clinic' kupitia gari la kutolea
huduma za dharura ambalo wahudumu wa afya huwafuata wananchi katika
maeneo yao, aidha kipaumbele cha matumizi ya gari hilo yamewekwa kwenye
maeneo ya pembezoni hasa maeneo ya kata za Oldonyowas, Oldonyosambu na
Olkokola, Bwawani, Oljoro na Laroi pamoja na maeneo mengine
itakapohiajika huduma ya dharura.
Hata hivyo, Wauguzi hao, wameadhimisha siku yao rasmi huku
halmashauri ikifanya vizuri kwa wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya
Jamii 'CHF' na kuwa halmashauri ya kwanza kati ya halmashauri 7 za
mkoa wa Arusha, kwa kufikisha asilimia 50.3% , hivyo wananchi wake,
kuwa na uhakiki wa matibabu pindi wanapougua, huku serikali ikielekea
kuimarisha mfuko huo na kuwa na Mfuko wa ya Jamii ulioboreshwa,
itakayowawezesha kutibiwa kuanzia Zahanati mpaka hospitali ya mkoa.
Ameendelea kufafanua kuwa halmashauri kupitia mapato yake ya ndani,
imewakatia vitambulisho vya 'CHF' wazee 692 na kuwahakikishia matibabu
rahisi na ya haraka, kwa kuwa na dirisha la wazee kwenye vituo vya afya
na hospitali zenye idadi kubwa ya wagonjwa.
Ndani ya halmashauri hiyo kumejengwa hospitali ya kimataifa ya
Maternity Africa katika eneo la Ngaramtoni ya Chini, hospitali
itakayotoa huduma bure za mama na mtoto pamoja na matibabu ya ugonjwa
wa Fistula.
Wauguzi hao pia wamesherehekea siku yao, huku serikali ya awamu ya
tano ikiongeza bajeti ya dawa mpaka kufikia bilioni 639 kutoka bilioni
29 ya hapo awali, jambo litakalowawezesha wauguzi kutoa hudumia kwa
kujiamini kwa wagonjwa na wateja wao.
Wauguzi halmashauri ya Arusha wameadhimisha siku hiyo kwa kutoa
huduma zaidi ya 10 bure kwa siku nne kabla ya kufikia kilele cha siku
hiyo tarehe 12 mwezi Mei, kwenye kituo cha Afya Nduruma huku wananchi
wa maeneo hayo kujitokeza kwa wingi kupata huduma hizo.
Muuguzi mkuu, halmashauri ya Arusha Sista Agusta Komba amesema kuwa,
mwitikio wa wananchi umekuwa mkubwa kutokana na uhaba wa huduma hizo
katika maeneo hayo na kuongeza kuwa wananchi wamejitokeza kwa wingi
katika siku zote nne na wamepata huduma hizo na muda si mrefu watakadhi
ofisi ya kijiji idadi kamili ya watu walihudumiwa kwa siku hizo.
Yohana Faustine moja ya wagonjwa aliyefika kupata huduma siku hiyo
amesema kuwa, wamefurahishwa na huduma za bure zilizotolewa kituoni hapo
huku akithibitisha sherehe kama hizo hazijawahi kufanyika katika maeneo
yao, wamekuwa wakizisikia kwenye vyombo vya habari, na kuishukuru
serikali ya awamu ya tano kwa kuwajali wananchi wa vijijini wa hali ya
chini kama wao.