MFAHAMU KOCHA MPYA WA SIMBA BAADA YA JULIO PAMOJA NA KING KIBADENI KUTIMULIWA

Na Mwandishi Wetu, Kariakoo
SULEIMAN Abdallah Matola sasa anakuwa Kaimu Kocha wa Simba SC baada ya makocha wote, Alhaj Abdallah Athumani Seif ‘King Kibadeni’ na Msaidizi wake Jamhuri Kihwelo ‘Julio’ kusimamishwa.
Matola ambaye kwa sasa ni Kocha Mkuu wa Simba B, atakuwa Kocha Msaidizi wa kocha mpya wa kigeni, atakayetambulishwa Desemba 1, mwaka huu.
Kocha mpya; Suleiman Matola anakaimu Ukocha Mkuu Simba hadi hapo kocha mpya atakapotambulishwa Desemba 1, mwaka huu. 

Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Simba SC, Joseph Itang’are ‘Kinesi’ amewaambia Waandishi wa Habari leo mchana makao makuu ya klabu, Mtaa wa Msimbazi kwamba, pamoja na kuwasimamisha makocha hao kwa kutoridhishwa na uwezo wao, pia wamemsimamisha Mwenyekiti, Alhaj Ismail Aden Rage kwa madai hawana imani naye.
Kinesi alisema uamuzi huo ulifikiwa katika kikao cha Kamati ya Utendaji kilichofanyika jana Dar es Salaam.
Kinesi amesema sasa yeye ndiye atakaimu Nafasi ya Uenyekiti wa klabu hadi hapo Mkutano Mkuu utakapofanyika.
Ikumbukwe Kinesi alichaguliwa kama Mjumbe tu wa Kamati ya Utendaji na Makamu Mwenyekiti ni nafasi ambayo anakaimu baada ya kujiuzulu kwa Geoffrey Nyange ‘Kaburu’. 
Hata hivyo, Rage hakuwepo kwenye kikao cha Kamati ya Utendaji jana na Kinesi alipoulizwa alisema kiongozi huyo yupo safarini.
 
habari kwa hisani ya BIN ZUBEIRY blog

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post