OFOO SARO ATOA SHUKRANI KWA KANISANI

Mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha ITV, Ufoo Saro akisoma somo kwenye biblia  wakati wa ibada maalumu ya shukrani kwenye Kanisa la (KKKT ) Usharika wa Kibamba nje kidogo ya Jiji la Dare Salaam jana. Picha na Sanjito Msafiri.  

MTANGAZAJI wa Kituo cha Televisheni cha ITV, Ufoo Saro ambaye alijeruhiwa kwa kupigwa risasi na mzazi mwenzake, Anthery Mushi, amefanya ibada na kusema: “Namshukuru Mungu kwa kumponya.”


Ni mara ya kwanza Saro kuzungumza tukio hilo tangu aliporuhusiwa kutoka Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu, MOI ya Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa amelazwa.
Katika ibada hiyo iliyofanyika katika Kanisa la Kilutheli Tanzania (KKKT) Usharika wa Kibamba, Jimbo la Magharibi, Ufoo huku akitokwa na machozi na wakati mwingine kushindwa kuzungumza alisema: “Ni miujiza tu ya Mungu yeye kunifanya mimi kuwa hai leo.”
Mtangazaji huyo ambaye alilazwa kwa zaidi ya wiki mbili, aliwashukuru watu wote waliomtia moyo, kumsaidia kipindi chote alichokuwa mgonjwa.
“Sina cha kuwalipa, ninawashukuru sana kwa wema wenu, pia kwa kuniombea. Mungu ni mkubwa na amenipigania, naendelea vizuri kwa sasa,” alisema na kuongeza:
“Mungu alinisimamia na nyinyi pia mliniombea, hakika sina budi kushukuru kwa kila jambo. Nitasoma zaburi ya 146 katika Biblia Takatifu ili kumshukuru Mungu kwa kunisaidia.”
Ufoo alisema kuwa ameamua kumshukuru Mungu kwa sababu siyo watu wote wanaopata matatizo kama yake wanapona.
Mchungaji aliyeongoza misa hiyo iliyoanza saa 4 asubuhi hadi saa 7 mchana, Joseph Maseghe alisema Mungu hakupanga Ufoo afariki dunia kwa kupigwa risasi.
“Mungu bado anakuhitaji, hakupanga ndiyo maana upo nasi leo. Hautakiwi kulia huu ni mwanzo wa maisha yako mengine, usilie unachotakiwa ni kumshukuru Mungu kwa kila jambo,” alisema.
Misa hiyo ilihudhuliwa na watu mbalimbali wakiwamo wafanyakazi wa ITV pamoja na Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Grace Kihwelu, Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), John Heche.
Baada ya kumalizika kwa misa hiyo, ndugu na marafiki wa karibu wa Ufoo walialikwa na mtangazaji huyo katika hafla fupi ya chakula cha mchana.
Akizungumza wakati akiwakaribisha wageni katika chakula cha mchana, alisema: “Nimepata pigo kubwa katika maisha yangu, familia yetu sasa haina baba wala mama, kweli namshukuru Mungu na nawaombea kwa Mungu wote walioniombea na kunitakia mema, sijui nimpe nini Mungu, sijui kwa kweli.”MWANANCHI.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post