Mfanyabiashara wa Madini ya Tanzanite,Vailet Matias (37), Mkazi
wa Njiro Arusha aliyepigwa risasi na polisi Oktoba 31 mwaka huu mkoani
Arusha, amehamishiwa Chumba cha Wagonjwa Mahututi (ICU) katika Hospitali
ya Arusha Lutheran Medical Center inayomilikiwa na Kanisa la Kiinjili
la Kilutheri Tanzania (KKKT).
Mfanyabiashara huyo alipigwa risasi baada ya
kudaiwa kutaka kumpiga risasi polisi aliyekuwa lindoni, akitumia bastola
yake kutokana na malumbano ya maegesho ya magari. Awali alikuwa
amelazwa katika Hospitali ya Mkoa ya Mount Meru, akiwa chini ya
uangalizi mkali.
Kaimu Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dk Paulo
Kisanga alisema jana kuwa Vailet alihamishiwa chumba cha wagonjwa
mahututi tangu juzi kutokana na hali yake kuwa mbaya kutokana na jeraha.
“Ni kweli huyu mgonjwa yupo ICU, mimi nipo nje ya
hospitali ila kabla ya kuondoka nilimwacha akiwa katika chumba hicho
akipatiwa matibabu” alisema Dk Kisanga.
Taarifa ya Dk Kisanga ilitolewa wakati kukiwa na
uvumi wa kufariki kwa mfanyabiashara huyo, ambao jana ulisambaa katika
maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas alisema jana kuwa alikuwa hana taarifa kamili za afya ya mgonjwa huyo.
Alisema awali baada ya mfanyabiashara kuegesha
gari hilo mbele ya lango kuu la kuingia katika Tawi la Benki ya CRDB,
alitakiwa kulitoa na akagoma ndipo polisi walilitoa upepo na kwamba
alipokuta limetolewa upepo ndipo alipoanza kulumbana na polisi hadi
akapigwa risasi.
CHANZO;MWANANCHI.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia