Balozi
wa China Liu Jieyi ambaye nchi yake ni Rais wa Baraza Kuu la Usalama la
Umoja wa Mataifa kwa mwezi huu wa Novemba, akielezea yale yaliyojiri
wakati wa mkutano wa Baraza Kuu la Usalama uliofanyika jana alhamisi na
kujadili hali ya Jamhuri ya Kidemokrasia. Tamko la Rais wa Baraza ambalo
limeridhiwa na wajumbe wote 15 wanaounda Baraza la Usalama, wametoa
wito kwa makundi ya waasi katika DRC kuweka chini silaha zao, makundi
hayo ni pamoja na kundi la M23. Mbali ya kuweka silaha chini yametakiwa
pia kuvunjika. Vivile Baraza hilo pamoja na kutambua kwamba kundi la
waasi la M23 limemwaga damu ya wananchi wengi wa DRC pia limepoteza
maisha ya walinzi wa amani wanaohudumu katika Misheni ya MONUSCO na kwa
sababu hiyo Baraza limerejea wito wake kwamba litaendelea kuunga mkono
walinzi wa amani maarufu kama Blue Helmet katika utekelezaji wa majukumu
yao.
Na Mwandishi Maalum
Baraza
Kuu la Usalama la Umoja wa jana alhamis limetoa wito linaolitaka
kundi la wapiganaji la M23 kuvunja kundi hilo mara moja ikiwa ni pamoja
na kuweka silaha zao chini.
Aidha
Baraza hilo limekaribisha tamko la awali la kundi hilo la M23 kwamba
limeamua kumaliza uasi wake na umwagaji damu dhidi ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo.
Katika
mkutano wake ulIojadili hali katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo, Balozi Liu Jieyi wa China ambaye ndiye Rais wa Baraza Kuu
la Usalama kwa mwezi huu wa Novemba na akizungumza kwa niaba ya
wajumbe 15 wa Baraza amesema.
“Baraza
linatoa wito wa hitimisho na utekelezaji wa makubaliano ya mazungumzo
ya Kampala ambayo pamoja na mambo mengine yanatoa fursa ya
upokonyaji wa silaha na kuvunjwa kwa kundi la M23 na uwajibikaji kwa
wakiukaji wa haki za binadamu.
Mazungumzo
hayo ya Kampala maarufu kama ‘Kampala Talks’ yanafanyika chini ya
usimamizi wa Mwenyekiti wa Mkutano wa Kimataifa wa Eneo la Maziwa Makuu,
( ICGLR), Rais Yoweri Kaguta Museven pamoja na Waziri wa Ulinzi wa
Uganda, Crispus Kiyonga.
Kwa
mujibu wa taarifa ya Rais wa Baraza Kuu la Usalama ( Presidential
Statement ) Baraza hilo limeonyesha wasi wasi kuhusu mwendelezo wa
tishio la usalama kutoka kundi la Forces Democratique de Liberation du
Rwanda ( FDLR).
Kutokana
na wasi wasi huo, Baraza Kuu linahimiza umuhimu wa kusambaratishwa
kwa kundi hilo pamoja na makundi mengine yenye silaha.
Aidha
Baraza Kuu la Usalama , limelaani kwa nguvu zake zote kuhusu
kuendelea kwa vitendo vya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu,
unaofanywa na makundi yenye silaha yakiwamo mauaji ya papo kwa
papo, unyanyasaji wa kijinsia na matumizi makubwa ya watoto katika
vita.
Vile
vile Baraza hilo pia limetambua kuwa katika kipindi cha miezi 19
ya uasi wa kundi la M23, kundi hilo limeua walinzi wa Amani wa Umoja wa
Mataifa wanaohudumu katika DRC kupitia Misheni ya Kutuliza Amani
maarufu kama MONUSCO inayoongozwa na Bw. Martin Kobler, ambaye ni
Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika DRC.
Na kwa
sababu hiyo Baraza Kuu la Usalama limerejea tena wito wake kwamba
litaendelea kuwaunga mkono walinzi wa Amani wa Umoja wa Mataifa,
maarufu kama Blue Helmet katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kundi
la M23 ambalo hivi karibuni lilipata kichapo cha aina yake kutoka
MONUSCO linaundwa na wanajeshi ambao waliasi kutoka jeshi la kitaifa
la DRC mwezi wa Nne,kundi ambalo pamoja na makundi mengine yenye
silaha yamekuwa mara kwa mara yakipambana na majeshi ya serikali
(FRDC).
Katika
mwaka uliopita mapigano kati ya makundi ya waasi na majeshi ya
serikali yalisababishwa zaidi ya watu 100,000 kuyakimbia makazi yao na
hivyo kuongeza uzito wa jukumu la kutoa misaada ya kibinadamu katika
eneo ambalo tayari zaidi ya watu 2.6 milioni ni wakimbizi wa ndani huku
wengine 6.4 milioni wakihitaji msaada wa chakula na huduma za
dharura.
Aidha
Baraza Kuu linahimiza Umoja wa Mataifa, na washirika wake wengine
kuendelea na jitihada zake katika utekelezaji wa Mpango Mpana wa
Kisiasa kwaajili ya DRC na Maziwa Makuu uliosainiwa na nchi 11 na
wadhamini wanne mapema mwaka huu , mpango unaolenga katika kuleta
Amani ya kudumu katika eneo la Maziwa Makuu.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia