ALIYEKUWA mgombea urais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania
kupitia Chama cha ADC, Chief Lutayosa Yemba, ametangaza kugombea kiti cha Spika
wa bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania kupitia chama cha ADC.
Chief Yemba, ameyasema hayo leo jijini Arusha, alipokuwa
akizungumza na vyombo vya habari akitoa tathimini ya uchaguzi mkuu uliofanyika
Oktoba 25 mwaka huu, pamoja na kutathimini uchaguzi wa jimbo la Arusha ambao
unatarajiwa kufanyika Desemba 13 mwaka huu.
Amesema baada ya kuanguka kwenye urais, sasa anaelekeza
nguvu zake kwenye Usipika, ambako ana uhakika wa kushinda kuwa ana sifa na
vigezo na ana imani atashinda kwa kuwa
anaungwa mkono na wabunge wengi wakiwemo wa CCM.
Aidha,ametumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wa Arusha kwa
kumpigia kura 200 kwenye uchaguzi mkuu uliopita licha ya chama chake kuwa ni
kichanga na sasa anafanya kazi ya kukijenga mkoani humo.
Amesema uchaguzi mkuu umekwishana tayari mgombea wa ccm,
Dakta John Magufuli, ndie rais na ADC, inamtambua na inampongeza kwa ushindi
huo na hivyo itashirikiana nae na Pia ADC ingelimtambua mgombea yeyote ambae
angelishinda kwenye uchaguzi mkuu Oktoba 25 mwaka huu.
Kuhusu marudio ya uchaguzi wa Zanzibar, Chef Yemba, amesema
ADC, itashiriki kwenye uchaguzi huo ambao ulifutwa kutokana na kugubikwa na
kasoro nyingi na kutabiri kuwa ADC, itakuwa ni sehemu ya serikali ya Zanzibar
kwa kuwa itapata ushindi mkubwa .
Ameiomba serikali ya mapinduzi Zanzibar, kuvunja tume ya
taifa ya uchaguzi na kuunda nyingine
itakayosimamia haki kwa wagombea
wote na kuepuka kasoro zilizojitokeza zisijirudie na kuvuga uchaguzi .
Amesema kwenye uchaguzi uliopita mawakala wa ADC, walizuiliwa kuingia kwenye vituo vya uchaguzi
kwa ajili ya kuhakiki zoezi zima la uchaguzi mkuu na kushangazwa na vituko vya
matokeo Pemba ambapo yeye Chief
Yemba,alipata kura nyingi zaidi kuliko mgombea urasi wa Zanzibar, Hamad Rashid,
ambae Pemba ndio ngome yake alipata kura 114 lakini ilijaziwa kura 4 wakati yeye akipata kura 90.
Kuhusu uchaguzi wa
ubunge jimbo la Arusha, ameipa ccm 38% Chadema 30 na ACT wazalendo 6%, na
kusema kuwa huo ni kwa mjibu wa utafiti alioufanya wa kuzungumza na makundi
mbalimbali ya wananchi wakiwemo waztu wazima vijana na wanawake.
Ameongeza kuwa hata hivyo ushindi utaamuliwa na kundi la
waswahili ambalo mpaka sasa halijatoa mwelekeo wa nani wamuunge mkono.
Yemba, amesema ADC katika uchaguzi huo haifungamani na chama
chochote bali inahitaji mbunge na sio
chama cha siasa .
Amesema kinachohitaji kwa Arusha ni kupata mbunge bora makini atakaezungumzia namna ya
kuboresha huduma za afya ,elimu na sio
kusuguana na serikali ili Arusha iweze kusonga mbele katika maendeleo.
“Umefika wakati wanasiasa kuachana na siasa za misuguano
kati ya wanasiasa na viongozi wa serikali ili Arusha iweze kusonga mbele”alisema
yemba.
Ameongeza kuwa mbunge wa Arusha, anayetetea kiti chake ameshindwa kufanya
mabadiliko ya maendeleo na badala yake
amejenga chama chake ,wananchi wanahitaji mbunge wa kuwasemea na sio chama cha
mtu.
Yemba, Amesema ADC,ilikuwa inategemea kuona wananchi
wakiandamana kupinga bei ya maji kupanda licha ya kuandamana kwa ajili ya
kukosekana kwa maji pekee.