WAKULIMA WALALAMIKIA WACHAKACHUAJI WA MBEGU

 Meneja Mauzo wa Kampuni ya Mbegu ya SEEDCO Kanda ya Kaskazini  Daniel Mwambugi  akitoa maelezo juu ya Mbegu za mahindi za kampuni hiyo zinazostahimili ukame na kumuwezesha mkulima kupata mavuno mengi katika shamba darasa lilipo kata ya King`ori wilaya ya Arumeru mkoani Arusha


 Akiwaonyesha wananchi ambao ni wakulima waliouthuria shamba darasa la kampuni hiyo
 Habari picha na Woinde shizza,Arusha
Wakulima wa Kijiji cha King`ori wilaya ya Arumeru mkoani Arusha wamelalamikia baadhi ya wafanyabiashara wanaochakachua mbegu na kuwauzia wakulima mbegu feki zinazochangia kuzorota kwa kilimo na kuwakwamisha wakulima.

Wakulima hao Peter Kessy na Kanankira Mbise wamesema kuwa mavuno machache yaliyopatikana katika msimu huu wa mavuno yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na mbegu feki ,mabadiliko ya hali ya hewa pamoja na kupanda kwa bei ya pembejeo.

Wakizungumza katika shamba darasa lililoandaliwa na kampuni ya Mbegu ya Seedco wamesema kuwa tatizo la mbegu feki ,dawa feki na mbolea feki limekua likiwaumiza wakulima wengi kutokana na uelewa mdogo walionao juu ya pembejeo na matumizi yake.

Diwani wa kata ya King`ori  Peter Kessy anapendekeza kuwepo na vituo maalumu cha uuzaji wa mbegu katika vijiji na kata ili kuepuka tatizo la uchakachuaji wa mbegu linalowaathiri wakulima wengi.

Meneja Mauzo wa Kampuni ya Mbegu ya SEEDCO Kanda ya Kaskazini  Daniel Mwambugi  amesema kuwa kampuni hiyo inayosambaza mbegu bora za mahindi na mboga mboga imekua ikiingia mikataba na wasambazaji wa mbegu ili kuzuia uchakachuaji pia kuna alama ya utambuzi ambayo hutumika kutambua mbegu hizo hivyo amewataka wakulima kuwa makini katika ununuaji wa mbegu.

“Tunawashauri wakulima watumie mbegu zinazoendana na hali ya tabia ya nchi katika maeneo husika ili waweze kupata mavuno bora ,tunazo mbegu za muda mrefu na muda mfupi  lakini pia tunawahamasisha kutumia mbegu bora ambazo ni Seedco ili waweze kuvuna kwa wingi” Alisema Daniel

Meneja wa Seedco upande wa mbegu za Mboga mboga Joyce Mbise alisema kuwa kampuni hiyo imeanza kusambaza mbegu hizo tangu mwaka jana hivyo ni fursa kwa Watanzania kuchangamkia kilimo cha mboga mboga ili waweze kukuza kipato cha mkulima na kuboresha lishe ya familia.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post