Diwani wa Kata ya Kiborlon (Chadema) katika Manispaa ya Moshi, Frank
Kagoma ameonyesha ujasiri wa hali ya juu alipopambana na majambazi
waliokuwa na silaha za moto.
Alinusurika kuuawa baada ya majambazi hao waliokuwa na bunduki na bastola
kumfyatulia risasi sita alipokuwa akiwafukuza ambazo hata hivyo,
hazikumpata.
Tukio hilo ambalo lilionekana kama sinema, lilitokea mwishoni mwa wiki baada
ya majambazi hao kuvamia duka la jumla la kuuza mitumba linalomilikiwa na
Menti Mbowe na kupora Sh10 milioni.
Katika tukio hilo lililotokea saa tano asubuhi eneo la Kiborlon, majambazi hao
walimjeruhi kichwani mfanyabiashara huyo anayemiliki pia mabasi ya Machame
Safaris.
Hali ya majeruhi huyo inaendelea vizuri. Akisimulia tukio hilo, diwani huyo
alisema siku hiyo akiwa maeneo ya Kiborlon, alipigiwa simu kuwa
mfanyabiashara huyo amevamiwa na majambazi ndipo alipoendesha gari lake
hadi eneo la tukio.
“Nilipofika pale wale majambazi watatu ndiyo walikuwa wanatoka kwenye duka.
Nikampelekea gari yule aliyekuwa ameshika bunduki. Kuona hivyo akafyatua
risasi hewani,” alisema Kagoma.
“Yule mwenye bunduki akaingia uchochoroni kuelekea Barabara ya Stendi ya
Kidia. Mwenzake aliyekuwa na bastola naye akawasha risasi nyingine hewani
kunitisha,” alisema.
Baada ya hali hiyo, diwani huyo alilazimika kujificha kwenye gari na majambazi
hao walidandia pikipiki na kuanza kukimbia kuelekea Barabara ya Msaranga,
naye akawafuata kuelekea huko.
“Wakati huo tayari vijana wangu wa bodaboda wakawa nao wamesikia hilo
tukio tukaanza kusaidiana kuwafukuza lakini mbele kidogo pale Msaranga wale
majambazi wakasimamisha pikipiki yao umbali wa mita 30 kutoka nilipokuwa
na mmoja wao mwenye bunduki alifyatua risasi mbili na mwenye bastola risasi
mbili kuelekea uelekeo wangu.
“Nililazimika kujificha kwenye kiti, wale majambazi wakajua wameniua.
Wakapanda tena pikipiki ili watoroke. Nikawasha tena gari huku vijana wangu
nao wakinisaidia tukaanza kuwafukuza,” alisema.
Kagoma alisema majambazi hao walipita maeneo ambayo gari haliwezi kupita
wakaelekea eneo la Mabogini Moshi Vijijini hadi lango la TPC na baadaye
wakaelekea Rundugai wilayani Hai.
“Kuna eneo vijana wangu wanasema kulikuwa na vumbi sana, ndipo
walipowapoteza na majambazi wakatoroka kupitia njia ya reli ili kukwepa polisi
waliokuwa wakiwasubiri mbele,” alisema na kuongeza: “Hatukuwa na silaha,
lakini tulijitahidi kupambana nao kwa ujasiri. Tatizo nafikiri tulikosea kidogo.
Ilitakiwa wakati tukifukuzana nao tuwape polisi uelekeo wa majambazi.”
Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Wilbroad Mutafungwa alisema jana kuwa
Jeshi lake litatoa taarifa rasmi kwa wanahabari leo kuhusiana na msako
unaoendeshwa na jeshi hilo.
“Kuna mambo tumeyafanya tangu tukio hilo litokee lakini kesho (leo) saa sita
mchana tutatoa taarifa rasmi pamoja na mafanikio tuliyofikia hadi sasa.
Tunaendelea vizuri na upelelezi,” alisema.
Kamanda Mutafungwa, alitoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa jeshi
hilo ikiwamo kuwafichua wahalifu na mbinu wanazozitua akisema polisi
wamejipanga kukabili wimbi jipya la ujambazi.