Mkurugenzi wa kitengo cha Africa wa
JICA, Hideki Watanabe akielezea Jinsi JICA wanavyofanya shughuli za
Maendeleo Afrika
Mdau kutoka Namaingo Bi. Mariam akichangia
jambo
Mkurugenzi wa
Namaingo Bi.Ubwa Ibrahim akimwelezea jambo mwakilishi wa benki ya rasilimali
(TIB) walipokutana katika semina ya uwezeshaji mitaji kwa ajili shughuli za
maendeleo.
Watoa mada kutoka
mashirika na taasisi mbalimbali za kifedha wakijibu maswali kutoka kwa wadau
waliohudhuria semina hiyo.
Washiriki
wakifuatilia semina
Wajasiriamali wakubwa kwa wadogo wametakiwa
kujitokeza kwa wingi kutumia fursa zilizopo ili waweze kuwezeshwa mitaji ili
wawekeze katika shughuli za maendeleo ili kupunguza tatizo la ajira hapa nchini
na kusaidia juhudi za serikali na wadau kuleta maendeleo hapa
nchini.
Hayo yalisemwa na Balozi wa Japan hapa
nchini Bwana Masaharu Yoshida alipokua akifungua semina ya wadau wa maendeleo
iliyojadili uwezeshaji wa mitaji kwa wajasiriamali kwa ajili ya shughuli za
maendeleo iliyofanyika jana (5/6/2016) jijini Dar es Salaam.
Semina hiyo iliyoandaliwa na shirika la
ushirikiano na maendeleo la Japan (JICA) pamoja na taasisi ya sekta binafsi
hapa nchini (TPSF) ilihudhuriwa na mashirika na taasisi za kifedha pamoja na
wajasiriamali kutoka sekta binafsi.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, watoa
mada walionesha kuwa kuna fursa kubwa kwa watanzania wote walioamua kuwa
wajasiriamali kwa kufungua viwanda vidogo kwa vikubwa, wakulima na
wafanyabiashara kutumia mashirika na taasisi za fedha kujipatia mikopo nafuu
ili kuwezesha kukuza biashara na viwanda vyao na wanaweza kulipa kwa muda mrefu
kwa riba nafuu.
Semina hiyo ilibainisha kuwa changamoto
kubwa ni kutokua na taarifa kwa watanzania wengi na hivyo kuogopa kuwekeza kwa
kutumia taasisi za fedha jambo lililoungwa mkono na washiriki wengi kwani
imebainika kuwa ni asilimia 16 tu ya watanzania wanatumia huduma za kibenki
hivyo wameaswa kubadilika waweze kunufaika na mitaji ambayo ipo lakini hakuna
wanaokidhi vigezo ambapo wanaofuatilia na kunufaika ni watu
wachache.
Mwavuli wa wajasiriamali wa Namaingo
(Namaingo Business Agency) ni moja ya taasisi zilizohudhuria na ziliahidiwa
kupewa ushirikiano na wadau wote wa kuwasaidia kufikia malengo yao kwani mitaji
ipo na Namaingo inakidhi vigezo vyote vya kukopesheka kwani mpango kazi wake
uko kitaalamu na ushiriki wa serikali na taasisi zake unaifanya iwe mkombozi
kwa watanzania wengi maskini.
Akizungumza baada ya semina hiyo Mkurugenzi
wa taasisi hiyo Bi. Ubwa Ibrahim aliwataka watanzania wote wajitokeze kujiunga
na taasisi yake wawekwe katika mpango wa kuwarasimisha na kuwawezesha kuingia
katika mipango ya kuwainua kiuchumi kwani kuna mradi wa kijiji biashara ambacho
wanachama wanatarajia kukopeshwa ardhi, kujengewa nyumba za makazi, kukopeshwa
mradi uliokamilika (kilimo na ufugaji) pamoja na utaalamu na usimamizi wa mradi
husika.
"Kwa sasa tuko katika hatua ya utekelezaji ambapo
tarehe 28 mwezi huu tunasaini mikataba na serikali na wadau wengine Diamond
Jubilee. Naomba watanzania waje washuhudie na kusikia juu ya mradi ili waamini
maanake kuna watu wanaongea bila kutenda, mimi nawakaribisha waje waone
utendaji na tuwape ushuhuda wa hatua tulizokia kwenye mradi wetu wa kijiji
biashara ambapo serikali imetoa ekari 44,000 kwa ajili ya mradi huu. Maendeleo
hayakusubiri hivyo kila mtu achangamke aje atuone tumweke kwenye mpango rasmi"
alisema Bi.Ubwa.
Mwanasheria wa taasisi hiyo
aliyejitambulisha kwa jina moja la Bwana Payas alisema kila siku kuna mafunzo
katika vituo vya Namaingo vilivyopo Ubungo, Ukonga na Temeke ambapo alisema
wajasiriamali hupewa mafunzo kabla ya kuingizwa rasmi katika mpango wa
kampuni. "Namaingo tunawezesha
wajasiriamali kusajiliwa TRA, BRELA, TFDA, Bima ya afya, mifuko ya jamii na
kuwaunganisha wao kwa wao. Kila Jumamosi tunakaribisha wanachama wapya
wanaopewa maelekezo na kuelezwa juu ya mradi wetu mkubwa wa kijiji biashara
kilichopo Mbawa, Rufiji ambapo Namaingo inaratibu mradi huo pamoja na wadau wa
maendeleo tukisimamiwa na baraza la uwezeshaji chini ya ofisi ya waziri mkuu"
aliongeza.