Watu wengi wamekua na tabia ambazo ni kinyume na maadili, tabia
ambazo hata mzazi anashangaa mtoto wake amezipata wapi, lakini kwa
asilimia 80, tabia ya mtoto inajengwa na mzazi na mlezi kuanzia mimba
mpaka umri wa miaka mitatu.
Kutokana na uelewa mdogo wa wazazi na kushindwa kupembua mambo chanya
ya kumjengea mtoto katika umri huo,husababisha mtoto kushindwa
kujitawala na kutawala mazingira yanayomzunguka kiakili, kimwili,
kihisia na kisaikolojia.
Tafiti zinaonyesha kuwa elimu duni ya wazazi na walezi juu ya malezi
na makuzi ya mtoto husababisha udumavu kwa watoto kimwili, kiakili na
kisaikolojia.
Tabia anazokuwa nazo mtu mzima, ziwe mbaya au nzuri ni matokeo
yaliyojengeka kwa mtoto kuanzia kipindi cha mimba mpaka alipofikisha
umri wa miaka mitatu.
Ubongo wa mtoto, unategemea zaidi kupewa/ kujazwa vitu kutoka kwa
wazazi na walezi pamoja na watu wanaomzunguka kuanzia kipindi cha mimba
mpaka miaka mitatu ili uweze kukua na kumjenga mtoto huyu uwezo wa
utambuzi.
Hayo yamethibitishwa na Afisa Ustawi wa Jamii, halmashauri ya Arusha,
Beatrice Tengi, wakati akitoa mafunzo kwa wauguzi wa afya wa kitengo
cha huduma za mama na mtoto wa halmashauri ya Arusha na Jiji la Arusha,
yaliyofanyika kwenye ukumbi wa SEDHA Jijini Arusha.
Afisa Ustawi huyo na mwezeshaji wa mafunzo hayo amesema kuwa, wauguzi
waliopata mafunzo hayo, wanakwenda kutoa mafunzo juu ya vichocheo
changamshi muhimu kwenye makuzi ya mtoto kwa wazazi na walezi kila
wanapofika Kliniki kuanzia wakati wa kliniki ya mama mjauzito na mara
baada ya mtoto kuzaliwa mpaka miaka mitano.
Aidha Afisa Usatawi huyo amesema kuwa wazazi na walezi wanatakiwa
kuelewa umuhimu wa kufahamu mambo yakuzingatia katika hatua za malezi
na makuzi ya mtoto, kuanzia mimba mpaka miaka mitatu ndio yanayojenga
mtoto kuwa na tabia nzuri au mbaya.
Amefafanua kuwa katika kipindi cha mimba mpaka miaka mitatu,mtoto
anatakiwa kupewa elimu changamshi yenye vichocheo chanya, itakayoanza
kumjengea uwezo mtoto wa kukua kimwili, kiakili na kisaikolojia.
Kwa mtoto mpaka kufikia umri wa miaka mitatu, ubongo wa mtoto
unakuwa tayari umejaa kwa asilimia 80, asilima 20 iliyobaki, huongezeka
kwa kipindi kilichosalia cha maisha yake yote.
Hivyo katika umri huu ni jukumu la wazazi na walezi kuhakikisha
wanamjenga na kumjaza mtoto maadili mema yatatayomfanya mtoto kuwa na
mitazamo chanya itakayomuwezesha kufanikiwa katika maisha yake ya
baadae.
Vichocheo chanya kutoka kwa wazazi na walezi na vinamfanya mtoto
aweze kujitambua, kujiamini, kujifunza zaidi na uwezo wa kupembua mema
na mabaya, hivyo wazazi na walezi wana jukumu kubwa sana la malezi ya
mtoto mpaka atakapofikisha umri wa miaka mitatu" amesema Tengi.
Endapo mtoto atakosa vichocheo chanya ni dhahiri mtoto huyu atakua
hajiamini, uwezo mdogo wa kujifunza, hawezi kujitegemea, muoga na mwenye
wasiwasi na kuwa na mahusiano mabaya na jamii katika maisha yake.
Tengi ameongeza kuwa kipindi chote cha ujauzito mtoto anatakiwa
kujazwa mambo mema ikiwemo upenda na kujaliwa na baada ya kuzaliwa mpaka
miaka mitatu mtoto anapaswa kufundishwa mambo chanya ya kijamii.
Hata hivyo Tengi amethibitisha kuwa makosa yanayofanywa na wazazi na
walezi kwenye hatua za malezi na makuzi ya mtoto yanamadhara makubwa
sana kwa maisha ya mtoto hasa anapokuwa mtu mzima.
Amewataka wazazi na walezi kushirikiana katika hatua zote za makuzi
ya mtoto kwa kumchochea vichangamshi chanya na kuongeza kuwa wazazi ni
lazima kuzungumza na mtoto mambo mema, kuacha kutukana, kumsemea mtoto
mambaya badala yake kumuonyesha upendo zaidi, kumjali na kumfanya
ajitambue,ajiamini, ajithamini na kuthamini wengine kuanzia anapozaliwa.
0 Comments
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia