Shahidi wa kwanza katika kesi
ya madai inayomkabili raia wa nchini China,Xu Ling ameieleza mahakama ya kwamba
raia huyo alitumia jina la kampuni yao kufanya kazi za ujenzi katika kampuni ya
Bonnite Bottlers Ltd iliyoko mjini Moshi na kisha kuchukua malipo ya kiasi cha
zaidi ya sh,400 milioni.
Shahidi huyo ambaye ni mkurugenzi wa
kampuni ya ujenzi ya Woodmender Co,Ltd ,Amaniel Ndossa alitoa ushahidi wake mwishoni mwa wiki iliyopita
katika kesi hiyo nambari 2 ya mwaka 2017 mbele ya hakimu mkazi,Janeth Mawole wa
mahakama ya hakimu mkazi Moshi.
Akiulizwa swali na wakili wa upande
wa mashtaka ,Issa Mavura kwamba makubaliano baina ya kampuni yake na raia huyo
yalikuwaje shahidi huyo aliiambia mahakama hiyo kwamba walikubaliano na Xu Ling
atumie jina la kampuni yake na kisha amlipe
asilimia 10 ya fedha katika kazi aliyoifanya Bonnite Bottlers Ltd.
Shahidi
huyo aliieleza mahakama hiyo
kwamba katika makubaliano hayo pia walikubaliana kwamba Xu Ling ambaye
pia ni mkurugenzi wa kampuni ya Li Jun Development Ltd kwamba atalipa kodi
zote za mamlaka ya mapato(TRA) mara akishapokea malipo ya kazi hiyo .
Akijibu swali aliloulizwa na wakili
upande wa utetezi,Isaac Samson kwamba alijuaje ya kwamba mteja wake amelipwa
malipo ya kazi hiyo shahidi huyo alisema kwamba walipata taarifa kutoka mamlaka
ya mapato(TRA) mkoani Arusha kwamba Xu Ling alifika kulipa kodi ya ongezeko la
thamani(VAT).
Mbele ya mahakama hiyo shahidi huyo
alisema ya kwamba anatambua ya kwamba kuna taarifa iliyofunguliwa mbele ya
jeshi la polisi mkoani Arusha kuhusu raia huyo kughushi baadhi ya nyaraka za
malipo za kazi hiyo zikiwemo baadhi ya risiti za malipo(invoice).
Mara baada ya kumaliza kutoa ushahidi
wake hakimu Mawole alihairisha kesi hiyo hadi Mei 17 mwaka huu ambapo shahidi
mwingine upande wa mashtaka atafika mbele ya mahakama hiyo kuwasilisha ushahidi
wake.
0 Comments
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia