Halmashauri ya Arusha imeanza ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya
elimu, baada ya serikali kuongeza fedha nyingine kiasi cha sh milioni
480, fedha za mradi wa lipa kutokana na matokeo (Payment for Result
'P4R').
Fedha hizo zimekuja mara baada ya halmashauri hiyo, kukamilisha kwa
umakini na kwa wakati, mradi wa awali wa P4R wenye thamani ya shilingi
milioni 500.
Kiasi hicho cha fedha cha shilingi milioni 480, kimetolewa kwa ajili
ya ujenzi na ukarabati miundo mbinu ya shule kufuatia adhma ya serikali
ya awamu ya tano ya kuwa na shule zenye miundombinu na mazingira bora
ya kufundishia na kujifunzia.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, wakati akikagua maendeleo ya
miradi hiyo, Mkurugenzi Mtendaji halmashauri ya Arusha, Dkt. Wilson
Mahera amekiri kupokea kiasi cha shilingi milioni 480 na kueleza kuwa
fedha hizo zinatumika kwa shule za msingi na sekondari kwa mgawanyo
unaokaribiana.
Dkt. Mahera amefafanua mgawanyo wa fedha hizo kuwa, kiasi cha
shilingi milioni 227 zitatumika kwa shule za msingi, ambapo milioni 96
zinatumika kujenga vyumba vinne vya madarasa, kwa gharama ya shilingi
milioni 24 kwa kila darasa pamoja na kununua madawati katika madarasa
hayo.
Aidha shilingi milioni 96 nyingine zitatumika kusawazisha ikama ya
walimu na milioni 35 zitatumika katika ukusanyaji wa takwimu muhimu za
shule zote za msingi, takwimu zitakazosaidia kupata picha halisi ya hali
ya shule, wanafunzi na uendeshaji wa shule wenye lengo la kuendelea
kufanya maboresho katika suala zima la elimu shuleni.
Ameendelea kueleza kuwa kiasi kingine cha shilingi milioni 253
kinatumika kukarabati na kumalizia miundombinu ya maabara za sayansi
kwenye jumla ya shule 7 za sekondari pamoja na kujenga vyumba 5 vya
madarasa kwenye shule nne za sekondari.
Aidha Dkt. Mahera amethibitisha kuwa, miradi yote imeanza kutekelezwa
kwa kasi kwenye shule zote zilizoainishwa na kuongeza kuwa, kukamilika
kwa miundombinu hiyo ya shule, kutaongeza ufanisi na ari ya wanafunzi
kujifunza na walimu kufundisha, jambo ambalo anaamini litapandisha
kiwango cha taaluma katika shule hizo.
Naye Afisa Elimu Sekondari, halmashauri ya Arusha, mwalimu Sofia
Msofe amesema kuwa, kukamilika kwa maabara katika shule za sekondari
kutaleta tija na hamasa kwa wanafunzi kupenda masomo ya Sayansi kutokana
kujifunza kwa nadharia na vitendo pia.
"Mimi ni mwalimu wa Biolojia, masomo ya Sayansi bila kufanya kwa
vitendo ni kubahatisha, lakini once mwanafunzi akijifunza kwa nadharia
akafanya kwa vitendo ni rahisi kuelewa na kukumbuka, na zaidi kulipenda
somo" amesema Afisa Elimu huyo.
Nakuongeza kuwa awali masomo ya Sayansi yalikuwa yanafundishwa kwa
kufanya 'alternative to practical' jambo ambalo wanafunzi walikuwa
wanalazimika kukariri zaidi bila kuelewa, lakini uwepo wa maabara,
wanafunzi sasa watafanya kwa vitendo na kwa uhalisia zaidi jambo ambalo
licha ya kuongeza uwelewa wanafunzi pia hufurahia somo.
Awali fedha za P4R kiasi cha shilingi milioni 500, zilitumika kujenga
vyumba 8 vya madarasa ya kidato cha 5&6, ukarabati wa maabara za
sayansi, mabweni ya wasichana na vyoo kwenye shule za sekondari
Mlangarini na Mwandeti, mradi ambao ulikamilika kwa wakati na tayari
wanafunzi wanafaidika na matunda ya mradi huo.
0 Comments
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia