JIJI ARUSHA KITOVU CHA MAFUNZO YA HALMASHAURI ZINGINE
Halmashauri ya Jiji la Arusha imekuwa ikipokea wageni kutoka miji
mbalimbali ndani na nje ya nchi kwa ajili ya kujifunza mambo ya
kiutendaji na hiyo ni kutokana na sababu za kiufanisi katika utendaji wa
shughuli za kila siku zinazoigusa hasa jamii.
Halmashuri ya Jiji la Arusha imepokea wageni (Mameya, Mkurugenzi,
Madiwani na baadhi ya Watendaji) kutoka halmashauri ya jiji la Dar Es
Salaam ambapo lengo kuu la ziara yao lilikuwa ni kujifunza juu ya
usimamizi na uendeshaji wa Jalala la kisasa, usimamizi wa shughuli za
kitalii katika jiji la Arusha hasa maeneo yenye vivutio na usimamizi
pamoja na uendeshaji wa shughuli za Maegesho.
“Nimefarijika na ujio wenu katika halmashauri yetu na naamini mnayo
mengi ya kujifunza na pia hii ni fursa kubwa kwetu pia kwani sio tu
ziara ya kimafunzo bali ni muunganiko ambao una faida kubwa katika siku
za baadae” alisema Mkurugenzi wa jiji la Arusha Ndg. Athumani Kihamia
alipokuwa akitoa neno la ukaribisho kwa wageni.
“Kufuatia ziara yenu pia halmashauri yetu itaweza kubadilishana
uzoefu na nyie katika Nyanja mbalimbali za kiutendaji na pia halmashauri
yetu kuweza kujitangaza vizuri katika miji mingine hapa nchini na hata
nje ya nchi” aliongeza Kihamia.
Naye mstahiki Meya wa Jiji la Arusha Mhe. Kalist Lazaro ameipongeza
halmashauri ya Jiji la Dar Es Salaam kwa kuchagua Jiji la Arusha kama
sehemu yao ya kujiongezea ujuzi.
Pamoja na ziraya yao ya kimafunzo pia walipata fursa ya kutembelea bustani inayoishi ya Themi (Themi Living Garden)
ambayo katika historia hapo mwanzo ilikuwa kichaka cha wahalifu ila
baadae Halmashuri ya Jiji la Arusha iliamua kuhifadhi eneo hilo na kuwa
mahala pa mapumziko. Kwa sasa linasimamiwa na kampuni ya watu wa Itali,
Oikos baada ya kuingia nao mkataba wa maridhiano juu ya utunzaji wa
mazingira.
Kadhalika walipata fursa ya kutembelea mradi wa Shanga Shangaa ambao
unaendeshwa na watu wenye ulemavu mbalimbali waliowezeshwa kufanya
shughuli za utengenezaji wa bidhaa mbalimbali zinazotokana na vyupa,
shanga, magazeti na malighafi za zamani na kuzitengenezea bidhaa mpya
kwa ajili ya matumizi mbalimbali ya kila siku. Mradi huo ni rafiki wa
wazingira.
Aidha Halmashauri ya Jiji la Arusha pia imepokea Wataalam kutoka
Jiji la Mwanza, Manispaa ya Ilemela na Morogoro kujifunza masuala ya
usafi na mazingira sambamba na uendeshaji na usimamizi wa shughuli za
dampo la kisasa lilipo kata ya Murriet Jijini hapa mapema leo hii.
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia