NCHI ZA AFRIKA ZATAKIWA KUTUMIA RASILIMALI ZILIZOPO KATIKA NCHI ZAO NA KUACHA KUOMBA OMBA

Na Woinde Shizza,Arusha
Nchi za Afrika zimetakiwa kuzitambua na kuzitumia rasilimali zake yenyewe katika kujiongeza kimapato na kuzifanya zijitegemee  kwa  kuacha kutegemea misaada ya wahisani ambayo imekuwa ikicheleweshwa, jambo ambalo linachangia kuzifanya ziendelee kuwa maskini.

Kauli hiyo imetolewa jana na mwakilishi wa benki ya maendeleo ya Afrika(AfDB), Julie Ladel katika mkutano wa wadau wa maliasili na utalii unaofanyika jijini hapa na kuwakutanisha wataalamu wa maliasili kutoka nchi 19 za afrika.

Alisema kuwa nchi za afrika zinarasilimali nyingi ila zinashindwa kuzitambua  na kuzitumia ipasavyo na jinsi zitakavyoweza kuwanufaisha wananchi wake kwa kujenga miundombinu bora ya barabara,elimu na Afya.

Baadhi ya washiriki kutoka nchini Tanzania wameeleza umuhimu wa mkutano huo kwani kwa kipindi kirefu nchi za Afrika zimekuwa zikinufaika na maliasili zake chini ya asilimia 30 huku sehemu kubwa zikiwanufaisha wawekezaji.

Akizungumza kwenye mkutano huo, mkurugenzi wa taasisi ya maendeleo na mipango Afrika, ya jijini Dar es salaam  [AIDI] Profesa ,Pascal Mihyo  alisema kuwa  lengo la mkutano huo ni kutafiti mbinu za jinsi ya kunufaika na  maliasili zilizoko Afrika zikiwemo misitu,maji,mafuta na gesi,ambapo ni pamoja na usimamizi wa maliasili na ukusanyaji wa mapato.

Alisema kuwa endapo kutakuwa na usimamizi mzuri kutasaidia kuongeza mapato kwa nchi za Afrika kufanya shughuli zao za maendeleo ikiwemo kutengeneza miundombinu ususani kwa wakazi wa vijijini ambako ndipo maliasili nyingi zinapatika.

Aidha aliongeza kuwa utafiti uliofanya taasisi ya kuzijengea uwezo nchi za Afrika na  kufadhiliwa na Benki ya maendeleo ya Afrika ulionyesha kuwa baadhi nchi za kiafrika zinauwezo mdogo wa kusimamia maliasili zake katika kuhakikisha nchi hizo zinanufaika na maliasili hizo ikiwepo migodi na gesi.

Mkutano huo wa siku Tatu umefadhiliwa na benki ya maendeleo ya Afrika [AfDB] Kwa kushirikiana na taasisi ya kuzijengea uwezo nchi za Afrika [African capacity building foundation]yenye makao makuu Harare nchini Zimbabwe.


About Woinde Shizza

Mwandishi , Mjasiriamali na Mbunifu wa Mavazi. Email : woindeshizza@gmail.com , Instagram: woindeshizzablog.