WAFUGAJI NAISINYAI WATAKIWA KUWA WAJASIRIAMALI


Na Woinde Shizza,Simanjiro
Wananchi wa jamii ya wafugaji wanaoishi katika kata ya Naisinyai wilaya ya Simanjiro inayopakana na machimbo ya Tanzanite wameshauriwa kuanza kujikita katika ujasiriamali badala ya kutegemea mifugo pekee.

Mkurugenzi mwenza wa kampuni Tanzanite One,Faisal Juma alitoa wito huo jana wakati akitoa msaada wa sh 15 million kwa wanawake wa Kata hiyo ili kuanzisha chama cha kuweka na kukopa(SACCOs).

Juma alisema, wananchi wa Naisinyai wamepata fursa ya kuwa katika eneo ambalo yanachimbwa madini ya Tanzanite  hivyo ni muhimu  wanufaike nayo kwa kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali na kufanyabiashara ,kuchimba na kuuza  madini hayo.

"Sisi kama Tanzanite One tunawajibu kuwasaidia kuwa wajasiriamali kwani tunachimba madini katika kata yenu na huu ni msaada kwa wajasiriamali lakini bado tutaendelea kusomesha watoto wa Kaya masikini na kutoa Michango mingine"alisema

Alisema mabadiliko ya tabia nchi yameathiri sana mifugo hivyo ili kutoathiri maisha ya wafugaji wanapaswa kuwa na mbadala wa kidogo wa kuwasaidia kimaisha.

Awali mwenyekiti wa kijiji cha Naisinyai,Taiko Laizer alishukuru michango wawekezaji na kuwataka kupanua wigo wa kutoa ajira kwa wananchi wa Naisinyai hasa wanawake.

'Tunajua mmewapa ajira vijana wa hapa lakini tunaomba zinapotokea ajira hasa wanawake tuongezewe"alisema

Naye Diwani wa viti maalum Kata ya Naisinyai Paulina Masekeni aliahidi fedha waliopatiwa
Wanawake wa kata hiyo zitatumika kuanzisha vikundi vya ujasiriamali kama walivyo omba.

About Woinde Shizza

Mwandishi , Mjasiriamali na Mbunifu wa Mavazi. Email : woindeshizza@gmail.com , Instagram: woindeshizzablog.