MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Arusha, imetishia kuzifuta kesi mbili
zinazomkabili Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), ikiwemo
kesi ya kusambaza ujumbe unaomkashifu Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho
Gambo.
Uamuzi huo ulitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo,
Augustine Rwezile, baada ya upande wa mashtaka kuomba uongezwe muda wa
siku 60 kwa ajili ya kukamilisha upelelezi wa kesi hizo.
Akizungumza baada ya upande wa mashtaka kuomba siku hizo, Hakimu
Rwezile alisema kama upande wa mashtaka utashindwa kukamilisha upelelezi
baada ya siku hiyo, mahakama hiyo itachukua uamuzi wowote ikiwa ni
pamoja na kuifuta kesi.
“Naahirisha kesi hii hadi Novemba 15 mwaka huu, kwa ajili ya kuja
kusoma maelezo ya awali ya mtuhumiwa, lakini siku hiyo mkisema upelelezi
haujakamilika, mahakama itafanya uamuzi wowote ikiwamo kuifuta kesi
hii,” alisema Hakimu Rwezile.
Awali, Wakili wa Serikali, Blandina Msawa, alidai mahakamani hapo
kuwa bado hawajakamilisha upelelezi, hivyo hawataweza kumsomea Lema
maelezo ya awali na mahakama hiyo iwape muda wa siku 60 kwa ajili ya
kukamilisha upelelezi huo.
Kwa upande wake, Wakili wa Utetezi, John Mallya, alidai mahakamani
hapo kuwa upelelezi wa kesi hiyo ni rahisi kwani tangu Lema akamatwe na
polisi na kufikishwa mahakamani, simu yake ya mkononi inashikiliwa hadi
sasa.
“Upelelezi wa kesi hii uko ‘very simple’, kwani simu ya Lema mpaka
sasa mko nayo mnaichunguza. Kwa hiyo, nashangaa kwanini upelelezi
haukamiliki kwa wakati ili mteja wangu asomewe maelezo ya awali,”
alihoji Wakili Mallya.
Katika kesi ya kwanza, Lema anadaiwa kusambaza ujumbe unaomkashifu
Gambo kati ya Agosti 20 mwaka huu, mkoani Arusha, huku akijua ni kosa
kisheria.
Katika kesi ya pili, Agosti mosi hadi Agosti 26 mwaka huu, Lema
anadaiwa kurusha maneno ya sauti kwa njia ya mtandao wa WhatsApp
yanayodaiwa kukusudia kuishawishi jamii iandamane Septemba mosi mwaka
huu, huku akijua ni kosa kisheria.
0 Comments
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia