BREAKING NEWS

Tuesday, February 28, 2017

MWIJAGE: TAASISI ZINAZOHUSIKA NA UWEKEZAJI ZIACHE UKIRITIMBA

  Ramani ya kiwanda

  Wa kwanza kushoto mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, alhaj Magid Mwanga ,wa pili kushoto mkuu wa mkoa wa Pwani, mhandisi Evarist Ndikilo na Jack Feng mkurugenzi wa kiwanda, wa tatu kushoto ni waziri wa viwanda, biashara na uwekezaji Charles Mwijage na Ridhiwan Kikwete na Cliford Tandari wakiweka udongo kwenye jiwe la msingi.(picha zote na Mwamvua Mwinyi)



Na Mwamvua Mwinyi, Chalinze
Waziri wa biashara, Viwanda na Uwekezaji, Charles Mwijage, amezitaka taasisi zinazohusika na uwekezaji kutokuwa na ukiritimba ili hali kufikia malengo ya serikali ya kukuza sekta ya viwanda.
Aidha ameeleza kwamba, wizara hiyo, imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji ambayo yatawezesha kuvutia wawekezaji wa ndani na nje.
Hayo aliyasema huko kitongoji cha Pingo Chalinze,Bagamoyo,wakati akiweka jiwe la msingi kwenye kiwanda cha Vigae cha Twyford Ceramics Ltd.
Mwijage alisema, uwekezaji huo unaendana na dhana ya Rais Dk John Magufuli wa kuifanya nchi kuwa ya Viwanda .
Alisema kwa kuanzishwa viwanda vingi vya aina hiyo kutasaidia kuongeza pato la nchi na kuzalisha ajira kwa wingi.
“Zipo idara ambazo zinafanikisha uwekezaji ikiwemo brela, idara ya uhamiaji, kazi, mamlaka ya mapato TRA, wizara ya ardhi, shirika la viwango TBS, baraza la Mazingira NEMC ambazo zinapaswa kufanya kazi kwa wepesi ili kufanikisha uwekezaji,” alisema Mwijage.
Alisema kati ya idara hizo baadhi zimekuwa zikifanya vizuri lakini nyingine zimekuwa zikiwapa usumbufu mkubwa wawekezaji.
“Wizara yangu haina tatizo lakini kuna baadhi ya idara zimekuwa kero na ukiritimba usio na sababu .,naomba kama kuna idara zinakuwa kikwazo niambieni ili tuwachukulie hatua,” alisema Mwijage.
Mwijage alisema nchi zilizofanikiwa kukuza uchumi wake kupitia viwanda zimeweza kutoa ajira nyingi kwa vijana kupitia sekta rasmi na isiyo rasmi.
Mkurugenzi mkuu wa kiwanda hicho Jack Feng alieleza, kiwanda hicho asilimia 95 ya malighafi itakuwa inatoka nchini ambapo kigae kinatumia maliahafi zaidi ya 10.
Alisema mara kiwanda hicho kitakapokamilika agosti mwaka huu kitaweza kupunguza asilimia 30 ya uagizaji wa vigae toka nje ya nchi.
Feng alisema wanatarajia kuajiri wafanyakazi 2,000 moja kwa moja na 4,000 kazi za muda na gharama ya mradi huo ni dola mil. 56 sawa na bil. 120 .
Alisema watauuza hadi nje ya nchi ikiwa ni pamoja na Zambia, Uganda, Rwanda na Burundi .
Nae mkurugenzi mtendaji wa kituo cha uwekezaji Cliford Tandari alisema kuwa uwekezaji wa kiwanda hicho ni wa mfano kwani utavutia makampuni mengi.
Alisema kwasasa kituo hicho kimeweza kutoa wigo mkubwa katika kuandikisha miradi mbalimbali toka china na kufikia miradi 667 ambayo itazalisha ajira 83,141 kwa watanzania ,miradi 452 ni miradi inayohusiana na sekta ya uzalishaji viwandani.
Mkuu wa mkoa wa Pwani Injinia Evarist Ndikilo alisema ,mkoa huo una viwanda 264 huku vikubwa vikiwa ni viwili.
Ndikilo alisema uwekezaji huo ni mkubwa na unatarajia kukuza ajira kwa vijana wa mkoa wa Pwani na Tanzania kwa ujumla.
Alisema mkoa wa Pwani bado una maeneo makubwa ya uwekezaji na tayari kuna eneo lenye ukubwa wa hekari 5,000 linahitaji wawekezaji .
Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete aliwapongeza wawekezaji hao kutoka nchi ya China .
Alisema Chalinze imejipanga kuwa sehemu ya uwekezaji ambapo kuna ujenzi wa viwanda mbalimbali.
Ridhiwani alisema kuwa changamoto kubwa inayokabiliwa wananchi na wawekezaji ni ukosefu wa maji,.
Alibainisha wamekuwa wakijitahidi kuikabili lakini bado hawajafanikiwa kuidhibiti aliomba wawekezaji hao kutoa ajira bila ya kuwabagua wenyeji.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates