Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Naibu Kamishna Charles Mkumbo
Na Rashid Nchimbi wa
Jeshi la Polisi Arusha
Jeshi la Polisi mkoani hapa limewataka wananchi kuwa makini
na kuchukua tahadhari zote katika kipindi hiki cha Masika. Akizungumza na
waandishi wa habari mchana wa leo ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Arusha Naibu Kamishna Charles Omari Mkumbo alisema katika kipindi hiki cha mvua
wananchi hawatakiwi kuvuka mito na mabonde yenye maji kwa hisia badala yake
wanatakiwa wawe na subira.
“Natoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Arusha katika kipindi hiki
cha masika hamtakiwi kujipa ujasiri na kuyakadiria maji ya mvua hivyo zinahitajika
tahadhari za kutosha dhidi ya watoto, au vyombo vyovyote vya usafiri kwani maji hayo huwa yanakwenda kwa kasi, yasubirini
yapite acheni hisia ili kuhakikisha maisha yenu hayahatarishwi na mvua”.
Alisisitiza Kamanda Mkumbo.
Kamanda Mkumbo alitoa wito huo baada ya jana usiku kunyesha
mvua kubwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huu na kusababisha vifo vya watu
saba. Alisema katika tukio la kwanza jana Usiku wa saa 4:00 katika kijiji cha
Kimbolo kata ya Enaboishu wilayani Arumeru, watu watano wote wakazi wa kijiji
cha Kyoga walifariki dunia baada ya gari aina ya Toyota Premio lenye namba za
usajili T 579 BSG kusombwa na maji.
Akiwataja watu hao waliofariki katika tukio hilo kuwa ni
Shengai Saiguran (30), Nembris Mungaya (20), Minis Loyi (25), Inoti George (40)
na Ngaisi Moluo ambaye umri wake bado haujafahamika mara moja huku dereva wa
gari hilo Yusuph Jacobo akinusurika.
Kamanda Mkumbo alisema mbali na vifo vya watu hao pia watu
wengine wawili walifariki dunia katika maeneo tofauti ambapo katika kijiji cha
Keriani mtu aitwaye Babu Robikeki alisombwa na maji kisha kufariki dunia wakati
anavuka mto wakati akitokea matembezini.
Wakati mtu wa saba ni
Seuli Meseyeki (37) dereva wa boda boda ambaye alikuwa anaendesha pikipiki aina
ya T-Better yenye namba za usajili T. 726 DFD naye alisombwa na maji eneo la
Olorieni Ngaramtoni wakati anavuka barabara. Pia pikipiki aina ya Boxer yenye
namba za usajili MC 892 ACR iliokotwa maeneo ya Olasiti kwa Mawala halmashauri
ya jiji la Arusha huku dereva wake hajulikani alipo.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia