Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Rais Dkt. John Magufuli hajawahi
kutangaza ama kutoa kauli ya kufutwa kwa vyama vya siasa nchini.
Ameyasema hayo leo Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali la
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe katika kipindi cha
maswali na majibu kwa Waziri Mkuu.
Mbowe amesema Rais Dkt. Magufuli alinukuliwa akisema atahakikisha
anafuta vyama vya upinzani ifikapo mwaka 2020 ata hakikisha hakuna
upinzani nchini, pia alitaka kujua nini kauli ya Serikali kuhusu
kunyimwa dhamana kwa Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ambaye
anashikiliwa kwa muda miezi mitatu.
Aidha, wakati akijibu swali hilo Waziri Mkuu amesema kuwa Rais Dkt.
John Magufuli hajawahi kutangaza kufutwa kwa vyama vya siasa ifikapo
2020.
“Kwanza nataka nikanushe kwamba Mheshimiwa Rais hajawahi kutangaza
kuvifuta vyama vya upinzani. Pia Watanzania wote wanajua nchi hii
inaongozwa kwa sheria, kanuni na taratibu,” amesema Waziri Mkuu.
Amesema kuwa wanaongoza nchi kwa kufuata mihimili mitatu ambayo ni
Serikali, Mahakama na Bunge na kwamba hakuna mhimili unaoweza kuingilia
mwingine.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amewahakikishia Watanzania kwamba suala la
upungufu wa sukari halitatokea nchini kwa sababu viwanda vya ndani
vinaendelea kuzalisha na hadi mwishoni mwa Januari vilifikia asilimia 86
ya uzalishaji.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia