WAZIRI NAPE AHAMASISHA WANANCHI KUTOA USHIRIKIANO KWA MAKARANI WA SENSA
Waziri
wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye
(kushoto), akizungumza katika kipindi cha Morning Trumpet cha
Televisheni ya Azam UTV, leo Agosti 15, 2022 jijini Dar es Salaam. Kulia
ni mtangazaji wa kipindi, Bw. Raymond Nyamwihula.
Waziri
wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye
(kushoto), akizungumza katika kipindi cha Pevuka cha Redio ya UFM, leo
Agosti 15, 2022 jijini Dar es Salaam. Kulia ni mtangazaji wa kipindi
hicho, Bw. Ramadhan Tuwa.

Waziri
wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye
(kulia), alipotembelea studio za kurushia kipindi cha michezo cha Azam
TV, leo Agosti 15, 2022 jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Meneja wa
Mitambo wa Azam TV, Bw. Raghvendra Tiwari,
Matukio
mbalimbali Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape
Nnauye (mwenye kaunda suti) alipotembelea ofisi za Azam Media Limited,
leo Agosti 15, 2022 jijini Dar es Salaam.
*********************
Na Mwandishi Wetu, WHMTH, DODOMA
Waziri
wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Nape Nnauye
amewataka watanzania kutoa ushirikiano kwa makarani wa Sensa ya Watu na
Makazi watakaopita kuchukua takwimu za watu na makazi siku ya taehe 23
Agosti 2022.
Waziri Nape ameyazungumza hayo leo Agosti 15, 2022
wakati wa alipotembelea kituo cha kurushia matangazo cha Azam Media
Group na kushiriki kipindi cha Morning Trumpet cha Televisheni ya Azam
UTV na kipindi cha Pevuka cha Redio ya UFM, jijini Dar es Salaam.
Amesema
kuwa kuna taarifa nyingi zitakusanywa na makarani wa Sensa kwa lengo la
kuisaidia Serikali kuweka mipango ya maendeleo inayozingatia idadi ya
watu na makazi ili kufikisha huduma za kijamii kwa wananchi kulingana na
uhitaji.
“Sensa ya Watu na Makazi ni jambo linalotokea mara moja
kwa miaka kumi, ni muhimu kila mwananchi kushiriki katika zoezi hili,
kwa kufanya hivyo utakuwa umejitendea haki wewe binafsi, jamii
inayokuzunguka na Taifa kwa ujumla kwa kuisaidia Serikali katika mipango
yake ya maendeleo”, Amezungumza Waziri Nape
Ameongeza kuwa
Serikali imedhamiria kuongeza ufanisi wa utendaji wake kupitia TEHAMA,
na kudhihirisha hilo, Sensa itakayofanyika tarehe 23 Agosti 2022,
itafanyika kidijitali kwa kutumia TEHAMA ambapo makarani wa Sensa
watatumia vishikwambi kuingiza taarifa za watu na makazi ambazo
zitaingia moja kwa moja kwenye mfumo.
“Tulikuwa tunatumia
makaratasi kujaza takwimu za Sensa, safari hii hatutumii makaratasi na
ndio faida ya TEHAMA, tutatumia vishikwambi kwa maana ya tablets na
taarifa na takwimu zitakazochukuliwa zitaingizwa kwenye mfumo”,
Amesisitiza Waziri Nape
“Takwimu zinaonesha zaidi ya asilimia 98
ya watanzania wanafahamu kuhusu Sensa inayoenda kufanyika, maandalizi ya
Sensa yamekamilika kwa asilimia kubwa, mwananchi ambaye hatashiriki
sensa hiyo atakuwa amejidhurumu haki yake lakini pia atakuwa hajaitendea
haki nchi yake”, Amesisitiza Waziri huyo
Imeandaliwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia