Baraza la Ardhi na Nyumba kata ya Mlangarini wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, limetupiwa lawama vikali kwa kupindisha haki na kushindwa kutii amri na maamuzi kutoka baraza la ardhi na nyumba la wilaya mkoani hapa.
Mkazi wa kijiji cha Kiserian Kata ya Mlangarini mkoani hapa,Godwin Massangwa ameibuka na kulishutumu vikali baraza hilo limekuwa likikiuka maagizo ya baraza la ardhi na nyumba mkoani hapa kufuatia kesi nambari 96 ya mwaka 2016 aliyoifungua dhidi ya wakazi 8 wa kata hiyo na kushinda kesi hiyo iliyokuwa ikihusu Migogoro wa Ardhi.
Hatahivyo,mwenyekiti wa baraza hilo,Julius Obedi alipohojiwa na gazeti hili kuhusu madai hayo alisema kwa kifupi kwamba Vyombo vya habari havina mamlaka ya kumhoji bali anapaswa kuhojiwa na baraza la ardhi na nyumba ngazi ya wilaya.
Katika hukumu ya kesi hiyo iliyoamriwa na mwenyekiti wa baraza hilo, David Mangure baraza hilo lilimpa ushindi mkazi huyo na kuamuru kuwa yeye ndiye mmiliki halali wa ardhi yenye ukubwa wa mita za mraba 995 katika kijiji kata ya Mlangarini.
Katika shauri hilo baraza hilo liliamuru washtakiwa Afred Lemeti,Lening'o Lemeti,Israel Lemeti,John Lemeti ,Meshiliek Lemeti,Piniel Saningg'o,Saiguran Lemeti pamoja na Lomayan Lemeti kupisha katika eneo la mkazi huyo walilolivamia.
Akihojiwa na gazeti hili Massangwa alisema kwamba baraza la ardhi na nyumba kata ya Mlangarini limekuwa likiitisha vikao kujadili mgogoro wa ardhi katika eneo lake bila kujali maamuzi ya kesi aliyoifungua nambari 96 ya mwaka 2016.
Massangwa alifafanua kwamba kumekuwa na upotoshaji na uporaji mkubwa wa haki unaofanywa na baraza hilo la kata ambapo kwa kiasi kikubwa baraza hilo limechangia migogoro ya Mara kwa Mara katika eneo lake badala ya kuwa sehemu ya utatuzi.
Alifafanua kwamba pamoja na baraza la ardhi na nyumba mkoani wa Arusha kumpa ushindi katika kesi aliyoifungua lakini baraza la ardhi kata ya Mlangarini chini ya mwenyekiti wake,Julius Obeid liliitisha kikao mnamo Mei 19 mwaka huu na kufanya maamuzi yanayopingana na mahakama za ardhi ngazi za juu.
"Kumekuwa na ukiukwaji mkubwa wa haki na upotoshaji unaofanywa na baraza la ardhi kata ya Mlangarini ambapo linekuwa likihitisha vikao na kupingana na maamuzi ya baraza la ardhi na nyumba mkoani hapa ambalo ndio ngazi ya juu" alisema Massangwa
Mkazi huyo alienda mbalii zaidi na kusisitiza kuwa pamoja na kushinda kesi ya rufaa kupitia wakili wake,Duncan Oola baada ya washtakiwa kukata rufaa ya kesi nambari 8 ya mwaka 2011 iliyosikilizwa na Jaji Aisha Nyerere katika mahakama kuu kanda ya Arusha, lakini baraza la ardhi na nyumba kata ya Mlangarini limeendelea kukaidi na kupuuza maamuzi hayo kinyume na sheria.
"Baada ya kushinda kesi niliyoifungua mwaka 2016 washtakiwa walikata rufaa nikashinda tena rufaa mahakama kuu lakini cha ajabu baraza la ardhi kata ya Mlangarini limeshindwa kuheshimu maamuzi hayo na wanaitisha vikao kupitisha maamuzi hayo kinyume na sheria" alisisitiza Massangwa
Massangwa aliiomba serikali kuingilia kati sakata hilo huku akidai kwamba amebaini baadhi ya viongozi wa baraza hilo wana maslahi na eneo lake na ana wasiwasi baadhi yao wamepewa chochote ili kumkandamiza.
Massangwa alimwomba rais Samia Suluhu Hasani kupitia mamlaka zake kumulika haya mabaraza ya kata ya Ardhi na nyumba ambapo baadhi ya wenyeviti wa mabaraza hayo wamekuwa wakijifanya Mungu watu na kukaidi maamuzi ya mabaraza ya juu au mahakama,kutokana na maslahi yao binafsi.
Aliongeza kuwa Baraza la Ardhi na nyumba kata ya Mlangalini wajumbe wa Baraza Hilo wanapotembelea eneo lenye mgogoro unapaswa kuwalipa kila mmoja sh,elfu 80, kuwatafutia usafiri,chakula pamoja gharama nyingine za kikao.