WAWEKEZAJI MTO WA MBU WAIOMBA SERIKALI KULITATHIMINI UPYA ENEO LA PORI TENGEFU LA LA MTO WA MBU


 


Kufuatia kuondolewa kwa wanyamapori kutoka eneo la pori tengefu la Mto-wa-Mbu, wawekezaji wanaondesha biashara za hoteli na kambi za utalii katika maeneo hayo wanaiomba serikali kulitathmini upya eneo hilo, na kufuta tozo kwani tayari sehemu hiyo imekosa sifa za kuendelea kuwa hifadhi.


Meneja wa uendeshaji wa Hoteli ya Kitalii ya Manyara Wildlife Safari Camp, Frank Benard Mbuya anasema kuwa eneo hilo tayari limekosa sifa ya kuendelea kuwa pori tengefu maana uhalisia umetoweka na hivyo hakuna sababu ya wao kuendelea kutozwa tozo za Kitalii za Game Controlled Area (GCA).


 



“Wageni wetu wanalizimika kulipa dola 30 za kimarekani, ambazo ni sawa na shilingi 70,000/- ingawa kwa sasa hakuna tena wanyama eneo hili, hivyo hatuoni sababu ya wageni wetu kuendelea kulipa gharama hizo,” alisema Mbuya.


 


Mapema mwaka huu, taasisi ya utafiti wa wanyamapori (TAWIRI), kwa kushirikiana na Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) waliwahamisha wanyama aina ya Pundamilia na Nyumbu kutoka pori tengefu la Mto-wa-Mbu, na kuwapeleka Tarangire, kufuatia mgongano kati wa wanyamapori na binadamu katika eneo hilo.


 


“Kwa sasa watu pia wamevamia eneo hili la pori kwa wingi na kuweka makazi yao kudumu,” alisema Maarten Breukink, mkurugenzi wa hoteli ya Manyara’s Secret.


 



Kwa mujibu wa Maarten eneo hilo limejaa vurugu za magari, pikipiki, mifugo, idadi kubwa ya watu, makazi holela na shughuli za kibiashara kiasi kwamba watalii hawapendi tena kwenda Mto-wa-Mbu.


 


Akizungumzia sakata Moja ya Maafisa wa Mamlaka ya Wanyamapori (TAWA) anaeleza kuwa tatizo la Mto wa Mbu ni la kisera Zaidi. Hivyo utatuzi wake uko katika ngazi ya kiwizara.


 


“Ni suala linalojumuisha wizara tatu,” alifafanua afisa huyo, akisema kuwa wizara za Maliasili, Ardhi na TAMISEMI zinahitaji kuketi pamoja kusuluhisha mgogoro huo, kwa sababu watendaji wa ngazi za chini wao wanatekeleza sharia zilizopo tu.


 



Aliongeza kuwa sharia ya Pori Tengefu bado haijafutwa, kwa hiyo yeyote anayejenga hoteli eneo hilo anawajibika kulipa tozo za GCA kwa wizara kupitia TAWA. Lakini pia tayari makazi ya watu katika eneo hilo yamerasimishwa kupitia sheria za vijiji chini ya TAMISEMI.



Katibu Mkuu wa wizara ya maliasili na utalii, Dokta Francis Michael amekiri kuwepo kwa muingiliano mkubwa wa shughuli za kibinadamu na uhifadhi katika maeneo mengi nchini na kwamba serikali imeanza kufanya tathmini ya baadhi ya maeneo kuangalia uwezekano wa kubadilisha au kurekebisha matumizi ya ardhi husika.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post