Mkuu wa wilaya ya Arusha, Said Mtanda amewafunda wastaafu watarajiwa mkoani hapa, kufanya matumizi sahihi ya fedha za mafao yao pindi wanapolipwa na kuacha kujiingiza kwenye starehe na kununua magari mabovu badala yake wajikite katika kuanzisha miradi vijijini au kuwekeza hisa kwenye mabenki
Pia aliwashauri kurudi kijijini kuanzisha miradi ya kisasa ya kilimo ,ufugaji na viwanda vidogo hatua itakayosaidia kunufaika na mafao yao kuliko kukimbilia kununua magari mabovu ya biashara au kujenga nyumba ya kupangisha jambo litakalopelekea kutapeliwa na kujikuta wakifilisika.
Kauli hiyo ameito wakati akifungua semina ya siku mbili ya wastaafu na wanachama wa mfuko wa hifadhi ya jamii NSSF , wapatao 300,semina iliyolenga kuwajenga kisaikolojia, ambapo pia aliwashauri kuhakikisha wanawekeza kwa kununua hisa kwenye mabenki na kujiweka salama na fedha zao.
Alisema kumekuwepo na tabia inayojitokeza kwa wastaafu pindi wanapolipwa mafao yao ambapo baadhi yao hujiingiza kwenye starehe na kuona vibinti vidogo ambao huwaibia fedha zao na muda mfupi huishiwa na kubaki wakihangaika hapa mjini.
Aliwataka wastaafu hao kutoogopa maisha mapya bali wazingatie kazi na matumizi sahihi ya fedha watakazolipwa kwa kwenda kuanzisha miradi vijijini au kuwekeza kwenye hisa kwenye benki
" Epukeni starehe za kuoa mabinti wadogo watakaowaponza na kufilisika au kwenda kununua magari mabovu ya biashara"alisema
Alisisitiza kuwa dhana ya kukimbilia kununua Magari ya biashara hususani Coaster ni ushauri mbovu kwa sababu wengi wao wanashauriwa bila kuwa na utaalamu wa biashara hiyo ,epukeni uwekezaji usio sahihi.
Awali meneja usimamizi wa mafao kutoka NSSF Taifa,James Galusoigo alisema semina hiyo inalenga kuwaanda wastaafu watarajiwa wanaokaribia kustaafu wenye umri kati ya miaka 55 hadi 60 ili kuhakiki kumbukumbu zao mapema baada ya ujio wa mfumo wa NIDA ili kuepuka kucheleweshewa mafao yao.
Alisema kuwa NSSF imefanya mabadiliko makubwa katika mfumo wake wa malipo ambapo mstaafu aliyekamilisha vema kumbukumbu zake atapokea mafao yake ndani ya mwezi mmoja baada ya kustaafu.
Kwa upande wake Josephat Komba meneja wa NSSF Mkoa wa Arusha,alisema semina hiyo ni fursa nzuri kwa wastaafu katika kuwajengea uwezo juu ya matumizi sahihi ya mafao yao .
Alisema washiriki wa semina hiyo ni wanachama wa mfuko wa NSSF kutoka kampuni na taasisi mbalimbali mkoa wa Arusha ambao wanatarajiwa kustaafu hivi karibuni
Alitoa wito kwa waajiri kuhakikisha wanawasilisha michango ya wafanyakazi wao kwa wakati ili kuepuka ucheleweshaji wa malipo ya mafao pindi wanapostaafu.