Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha imeahirisha kutoa hukumu ya aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai Mkoani Kilimanjaro Lengai Ole Sabaya na wenzake sita baada ya Hakimu Mkazi Mwandamizi anayesimamia shauri hilo dkt Patricia Kisinda kuwa na majukumu mengine .
Akiahirisha kutoa hukumu hiyo Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha Fadhili Mbelwa alisema ni sahihi kwamba shauri limefika kwaajili ya kutoa hukumu na kwakuwa lilikuwa linasikilizwa na Hakimu Mkazi Mwanamizi dkt Patricia Kisinda ambaye kwa siku ya leo yupo katika majukumu mengine hivyo hukumu hiyo itatolewa mnamo 10/6/2022 .
Sabaya na Wenzake walikuwa wakikabiliwa na kesi namba 27 ya uhujumu uchumi na utakatishaji fedha ambayo wanadaiwa kutenda mnamo tarehe 22/1/2021 kwa mfanyabiashara Francis Mrosso kwa kuchukua kiasi cha shillingi Milioni 90 .
Katika kesi hiyo washtakiwa wengine ni Enock Mnkeni ,Watson Mwahomange ,John Aweyo ,Sylvester Nyegu ,Jackson Macha pamoja na Nathani Msuya .