Ticker

6/recent/ticker-posts

MERU WAZINDUA KAMPENI YA NNE YA CHANJO YA POLIO

 

Na Woinde Shizza , ARUSHA

Halmashauri ya Wilaya ya Meru, Wilayani Arumeru imezindua rasmi kampeni ya siku nne kuanzia tarehe 18 hadi 21 Mei 2022 ya chanjo ya matone ya polio kwa watoto wenye umri chini ya miaka 5 .


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya  Meru Mwl.Zainabu Makwinya amesema kampeni hiyo ya utoaji chanjo ya polio itafanyika nyumba kwa nyumba na kuhimiza kila  mzazi/mlezi kuhakikisha watoto wanapata chanjo hiyo muhimu .

Aidha, Mwl.Makwinya amesema kampeni  ya chanjo ya Polio ni ya Kitaifa na inalenga kuongeza kinga mwili kwa watoto chini ya umri wa miaka 5 ili kuzuia maambukizi ya kirusi cha Polio, ikizingatiwa kirusi hicho kiliripotiwa  kuwepo nchi jirani ya Malawi. 

Aidha Mwl.Makwinya amewashukuru wadau waliochangia kufanikisha kampeni hiyo kwa kutoa magari na amewaagiza wataalum kuimarisha usimamizi wa utoaji huduma za chanjo kwa kipindi chote cha kampeni hiyo.

Mganga Mkuu Wilaya Dkt.Maneno Focus amesema chanjo ya Polio  ni muhimu sana  kwani ugonjwa wa Polio  unaosababishwa na kirusi ambacho huambukizwa kwa kula au kunywa kitu kilichochafuliwa  na kinyesi chenye vimelea  hauna tiba.

Miongoni mwa wazazi walio  hudhuria uzinduzi huo wamehimiza kila mzazi kuona umuhimu wa chanjo hiyo, Izack Pallangyo ametoa wito kwa wazazi  wa kiume kuwa mstari wa mbele kuhakikisha watoto wanapata chanjo hiyo "kinga ni bora ikizingatiwa, Polio haina tiba"amehimiza Ndg.Pallangyo

Naye Zenice Kiriho ambaye ni mama wa mtoto wa kwanza kupewa chanjo  wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo ameishukuru Serikali kuhakikisha chanjo ya polio inapatikana na kurahisisha utoaji wake ambapo mbali na kutolewa kwenye vituo vya tiba itatolewa nyumba kwa nyumba.

Uzinduzi huo wa Kampeni ya Chanjo ya Polio katika halmashauri ya Wilaya ya Meru umefanyika katika kituo cha Afya Usa-River ambayo  inalenga kuwafikia watoto 39,649 katika halmashauri ya wilaya ya Meru.

Post a Comment

0 Comments