ANGALIA JINSI NYATI MWEUPE ALIVYOKUWA KIVUTIO NDANI YA HIFADHI YA TARANGIRE

 

 

 




Idadi ya watalii wanaotembelea hifadhi ya Taifa ya Tarangire imeongezeka kufuatia kuonekana kwa nyati wawili wenye rangi ya ajabu katika hifadhi hiyo hivi Karibuni 



Kamishna msaidizi katika Shirika La Hifadhi za Taifa, (TANAPA) Ignace Gara amesema kuwa kwa sasa kila mgeni kutoka nje ya Tanzania anayeingia Tarangire anaulizia kuhusu uwepo wa Nyati weupe.


Lakini pia watanzania wengi wanaonesha shauku ya kuwaona Nyati wa kwanza kabisa wenye rangi nyeupe na tayari baadhi yao wameanza kutembelea Tarangire kuwaona wanyama hao.


“Hivi karibuni tulikuwa na wageni kutoka ufaransa ambao walitumia saa nyingi kumuangalia Nyati Mweupe jike, ambaye ni wapili kuonekana ndani ya wiki moja tu,” alisema Gara.


Tarangire inakadiriwa kuwa na Nyati wapatao 7000 kutokana na sensa iliyofanyika mwaka 2015.


Zoezi jingine la kuhesabu wanyamapori, linatarajiwa kufanyika tena hifadhini humo.


Kwa sasa kuna utafiti wa Tembo unaoendelea Tarangire kupitia taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori nchini (TAWIRI).


Kwa mujibu wa mhifadhi wa Tarangire, tayari watafiti kutoka taasisi hiyo pia wameonesha nia ya kuanza uchunguzi maalum kuhusu uwepo wa Nyati weupe pamoja na wanyama wengine wenye rangi tofauti hifadhini humo.


"Ndani ya hifadhi hii pia kumeonekana Nyani Mweupe, Twiga Mweupe na Swala Mweupe katika hifadhi ya Tarangire"alisema Gara


Askari wa uhifadhi, Tarangire Natey Joseph Zakaria anasema kuwa tofauti na Nyati wengine, maarufu kwa ukali, hawa wenye rangi nyeupe huwa ni wapole Zaidi.



“Na pia wao hupenda kujitenga na wengine ndani ya kundi kwa hiyo ama watakuwa mbele Zaidi au nyuma wakati wakiwa kwenye malisho.” Anasema.


Natey anaongeza kuwa Nyati hao weupe hawaonekani kirahisi kwa sababa wanaathirika sana na jua kali kwa hiyo huonekana asubuhi sana au jioni jua linapoanza kuzama.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post