MAFUNZO MAALUMU KWA WATAALAM

 


Mganga mkuu wa mkoa wa Arusha Dkt. Sylvia Mamkwe amefungua rasmi mafunzo ya utoaji huduma za magonjwa yasiyoambukizwa kwa watoa huduma za afya kutoka mikoa mitatu ya Arusha, Kilimanjaro na Singida.


Katika uzinduzi huo Dkt.Mamkwe ameishukuru serikali ya awamu ya sita kupitia Rais wake Mh.Samia Suluhu Hassan kwa kuboresha miundombinu mbalimbali ya afya na hasa mkakati huu unaoendelea sasa ambao ni kutoa mafunzo kwa watoa huduma hao wa afya.


Mganga Mkuu wa Mkoa  amewahimiza washiriki wa mafunzo hayo kushiriki kikamilifu na matokea ya mafunzo hayo yakaonekane  katika vituo vyao vya kazi.




Aidha Dkt.Mamkwe ameagiza waratibu wa  magonjwa yasioambukiza katika mikoa waandae taarifa kila robo ya mwaka na wazifanyie uchambuzi na mrejesho katika vituo vya afya ili kuweza kutatua changamoto zinazojitokeza kwa haraka.Pia ameomba waratibu hao kuwasilisha taarifa hizo katika mamlaka husika kimkoa na hata ngazi ya Wizara ya afya.




Dkt. James Kiologwe Mkurugenzi msaidizi kitengo cha huduma ya magonjwa yasioambukizwa taifa ameanisha kuwa 2/3 ya wananchi wanaishi na magonjwa yasiyoambukizwa bila kujijua hivyo mafunzo haya yatasaidia sana watoa huduma za afya kufanya uchunguzi na utambuzi wa haraka kwa wagonjwa. Aidha amewashukuru sana wadau wa afya kwa mchango wao wa kuwekeza katika kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza.




Bi.Valeria Milinga Meneja mpango wa Taifa wa Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa yasiyoambukiza ameainisha kuwa  Wizara ya afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tamisemi, Tanzania Diabetics Association(TDA), pamoja na wadau wengine wamekusudia kufikia mwaka 2023 wanatarajia kuwajengea uwezo  idadi ya wahudumu 2632 wanaotoa huduma hiyo kutoka katika vituo vyote vya afya  600  mikoa yote 26 Tanzania.




"Mpaka kumalizika kwa mafunzo haya serikali itakuwa  imefanikiwa kikamilifu kutoa mafunzo  kwa mikoa 5 ikiwemo Arusha Kilimanjaro na Singida na vituo vya afya 140 vitafikiwa na watoa huduma 510 watakuwa wamepatiwa mafunzo hayo". amefafanua Bi. Valeria.




Bi.Valeria ameainisha kuwa washiriki wa mafunzo hayo watafundishwa mbinu mbalimbalia za kuzuia magonjwa yasiyoambukizwa ikiwemo utoaji wa elimu ya lishe na mazoezi ya viungo.



Pia washiriki watajengewa uwezo katika kufanya utambuzi wa mapema kwa wagonjwa wa magonjwa hayo, elimu ya matibabu na namna ya kushirikiana na jamii kuwasaidia wagonjwa hao. 


Magonjwa yasiyoambukizwa yametajwa kuwa ni pamoja na kisukari, shinikizo la damu, magonjwa ya moyo, kupooza,magonjwa ya mfumo wa hewa,magonjwa ya afya ya akili, saratani na matibabu ya majeruhi wa ajali.

Mafunzo haya yatafanyika kwa siku 5 katika ukumbi wa mikutano AICC Arusha yakihudhuriwa na wadau mbalimbali wa Afya wakiwemo OR-TAMISEMI ,TDA, TANCDA, TANSDA, TTCF.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post