“KKKT ARUSHA BADO HAKIJAELEWEKA”

HALI ya hewa inadaiwa kuchafukua  katika kikao cha  kupokea taarifa ya ununuzi wa basi la kwaya ya kanisa la kiinjili la kilutheri (KKKT)Usharika wa Arusha mjini baada ya baadhi ya wajumbe wa kamati hiyo kuipinga vikali taarifa ya fedha iliyowasilishwa mezani  na mchungaji wa usharika huo,Titos Laroya kwa madai kuwa taarifa hiyo “imechakachuliwa” na kamwe hawana imani nayo.

Pia, baadhi wa wajumbe wa kikao hicho wanadaiwa kukataa ombi lililotolewa kikaoni hapo na mchungaji huyo la kukubali  kulipokea basi hilo la kwaya kwa kuwa litauzwa hapo baadaye kwa hasara baada ya miaka mitatu pindi likishatumika.

Hatua ya kikao hicho inafuatia baada ya waumini wa kanisa hilo pamoja  na wajumbe wa kamati ya ununuzi wa basi hilo  kupinga vikali ununuzi wake uliogharimu kiasi cha sh,54 milioni   ihali ni bovu huku wajumbe wa kamati ya ununuzi wa basi hilo wakipinga kwamba hawakushirikishwa katika mchakato wa ununuzi .

Kwa mujibu wa vyanzo vya habari vya gazeti hili vilidai ya kuwa kikao hicho kilifanyika mnamo  novemba 15 mwaka huu majira ya saa 6.00 jioni hadi saa 9.30 usiku kanisani hapo ambapo kilifanyika chini ya makamu mwenyekiti wa kamati ya mradi wa ununuzi wa basi hilo,John Mziray.

Taarifa hizo zinadai ya kuwa baadhi ya washiriki wa kikao hicho walikuwa ni Laroya na msaidizi wake,Lomayani Babu,wajumbe wa kamati ya ununuzi wa basi hilo,injinia Asili Munisi,David Tilya pamoja na waimbaji mbalimbali wa kwaya ya usharika huo.

Taarifa ndani ya kikao hicho zinadai ya kuwa hali ya hewa ilianza kuchafuka baada ya ,Laroya kuwasilisha taarifa ya fedha za ununuzi wa basi hilo kwa kutamka kuwa fedha zilizokusanywa katika harambee za uchangiaji wa basi hilo zilikuwa ni jumla ya kiasi cha sh,61,137,850 milioni.

Laroya,anadaiwa kuwasilisha taarifa ya gharama za ununuzi wa basi hilo na matengenezo yake kwa kutamka kuwa jumla ya fedha kiasi cha sh,54,913,202 milioni zilitumika huku akidai fedha zilizobaki hadi sasa ni kwenye akiba benki ni sh,6,224,648 milioni hali ambayo ilipingwa vikali na wajumbe hao.

Wajumbe  hao walidaiwa kupinga taarifa hiyo ya fedha kwa kudai kuwa taarifa hiyo imechakachuliwa kwa kuwa fedha zilizochangwa katika harambee mbalimbali za ununuzi wa basi hilo zilikuwa ni zaidi ya sh,72  milioni kitendo kilichopelekea Laroya kuwaomba msamaha kwa kuwasihi kuipokea taarifa hiyo.

Hatahivyo,ilidaiwa kuwa wakati mabishano hayo yakiendelea ndipo ilipomlazimu Laroya kuwaomba msahama wajumbe wa kikao hicho kwa kulikubali basi hilo hata kama ni bovu kwa kuwa uongozi wake utafanya juhudi  za kuliuza kwa hasara baada ya miaka mitatu likishatumika kitendo kilichoungwa mkono na mjumbe mmojawapo(Tilya).

“Jamani mtu mzima akishaomba msahama ana budi kusamehewa lazima mtambue kuwa kufanya kosa si kosa bali kurudia kosa ndio kosa kubalini tu taarifa hii“alinukuliwa Tilya na mjumbe mmojawapo lakini ushawishi wake ulidaiwa kupingwa vikali

Makamu mwenyekiti,Mziray ambaye alidaiwa kukisimamia kikao hicho alikiri kufanyika kwa kikao hicho huku akisema kuwa wajumbe wa kikao hicho waliipinga taarifa hiyo kwa madai kuwa hawana imani nayo huku akisisitiza kwamba hadi sasa hajui hatma ya sakata hilo.
 
Mchungaji  Laroya huyo alipotafutwa na gazeti hili kwa lengo la kuzungumzia madai hayo alisema kuwa kuwa yeye siyo msemaji wa dayosisi na kumshauri mwandishi wa gazeti hili kumtafuta Askofu mkuu wa kanisa hilo dayosisi mkoani Arusha,Thomas Laiser ambaye naye alikataa kuzungumzia madai hayo kwa kumtaka mwandishi wa gazeti hili kutofuatilia habari hizo.

“Hakuna ufisadi wowote bwana labda huo ufisadi uwe wa kwako wewe ,hili jambo linakuzwa tu nakuomba usinipigie simu tena….. ,tena nakuomba usithubutu kunipigia simu kuniuliza mambo hayo hata kama unanirekodi  sawa lakini usinipigie simu tena kuniuliza”alisema Laiser na kukata simu ghafla

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post