LEMA ASEKWA MAHABUSU



lema akiwa na wafuasi wake nje ya mahakama


MBUNGE wa jimbo la Arusha mjini kupitia tiketi Chadema,Godbless Lema  amesweka mahabusu katika gereza la Kisongo lililopo nje kidogo ya jiji la Arusha  baada ya kushindwa kukidhi masharti ya dhamana katika kesi  inayomkabili mbunge huyo ya kufanya maandamano , mkusanyiko usio halali na kuhamasisha watu kutenda kosa.

Mbunge huyo na wafuasi wake 18 wote kwa pamoja walifikishwa  katika mahakama ya hakimu mkazi mkoani Arusha ,mbele ya hakimu  Judith Kamala ,mwendesha mashtaka wa serikali,Augustino Kombe aliieleza mahakama kuwa watuhumiwa wote kwa pamoja walitenda  makosa hayo mnamo oktoba 28 mwaka huu.

Kombe,aliyataja makosa hayo kuwa ni njama ya kutenda kosa kinyume cha sheria ya kifungu nambari 384 na 385 cha kanuni ya adhabu,kosa la pili ni kufanya maandamano yasiyo halali ambayo yalianzia katika barabara ya mahakama ya hakimu mkazi mkoani hapa hadi kwa mkuu wa wilaya ya Arusha,zilipo ofisi za Mbunge huyo.

Alidai kuwa katika maaandamano hayo walikuwa waandamanaji zaidi ya 100 ambayo  yaliyoandaliwa  kinyume cha sheria kifungu  namba  74


Mwendesha mashitaka huyo alisema kuwa kosa la tatu linamkabili Lema peke yake ambaye anashitakiwa kwa kuhamasisha watu kutenda kosa,ambapo anadaiwa kuwa katika eneo la Clock Tower mbunge huyo alihamasisha watu kujipanga na kukataa amri iliyokuwa imetolewa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha (OCD(Zuberi Mwombeji,kinyume cha kanuni ya adhabu ya 390 na 35.

Kombe, aliieleza mahakama hiyo kuwa katika shitaka la nne linalowakabili watuhumwia wote 19 ni kutokubali amri halali ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha (OCD(, Mwombeji ambapo wanadaiwa kuwa katika eneo la Hoteli ya New Arusha ,wote kwa pamoja walijipanga na kukataa amri iliyowataka kutawanyika,kinyume cha kifungu cha 42(2( cha sheria ya polisi.

Shtaka la tano linalowakabili watuhumiwa hao  ni kufanya kusanyiko la watu lisilo halali,kinyume cha sheria ya polisi cha 45 na kifungu cha 14(1( na kanuni ya adhabu,wakidaiwa kuwa katika ofisi ya Mkuu wa wilaya zaidi ya waandamanaji 100 walikataa kutii amri za Mkuu wa Polisi wilaya ya Arusha ,OCD Mwombeji ya kuwataka watawanyike.

Kombe ,aliieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika hivyo unaendelea ambapo alimwomba Hakimu huyo kupanga tarehe ya kutajwa kwa kesi hiyo.

Watuhumiwa hao ni Lema,Joseph Simon,Dina Kamtoni,Musa Mwakilema,Jafari samweli,Juliana Lukumay,Gerald Majengo,Leonard Kiologo,Frank Daniel,Kelvin Simon na Hassan Mdigo.

Wengine ni pamoja na Lomayan Nasi,Rashid Shumbeti,Amedeus Chami,Daud Hamza,Meshack Betuel,Hamad shaban,Bahati Daud na Richard Mollel.
Kati  ya watuhumiwa hao walioweza kukidhi matakwa ya dhamana na kuachiwa huru na mahakama hiyo kwa dhamana ni Dina Anthony,Gerald Majengo,Hassan  Mdigo,Lomayan Nasi,Rashid Shchbeti,Daud Hamza na Bahati Daudi.

Watuhumiwa wote 19 walikana kutenda makosa kwa nyakati tofauti  na Hakimu Kamala kuihairisha kesi hiyo hadi Novemba 14 mwaka huu.



Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post