MKUU WA WILAYA MANYARA AWAASA WACHIMBAJI

MKUU wa mkoa wa Manyara,Elaston Mbwilo amewaasa wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite wa mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro kuungana vikundi ili waweze kujikwamua kutokana na vikwazo mbalimbali.

Mbwilo aliyasema hayo wakati akifungua mkutano wa eneo tengefu la Mirerani uliofanyika juzi kwenye ukumbi wa Manyara Inn uliopo mji humo ambapo alielezwa changamoto mbalimbali zinazowakabili wachimbaji wadogo.

Alisema suala la kuuziwa vifaa vya milipuko kwa bei ghali linaweza kumalizika kwa wachimbaji wadogo,endapo wachimbaji hao wataungana na kuunda kikundi ambapo wataweza kuwa na sauti moja.

“Kama mlivyosema hivi sasa mnakabiliwa na tatizo la zana za milipuko mnauziwa kwa bei ghali na pia wasambazaji wapo wawili tu nchi nzima,mnapaswa muunde umoja ili kukabili hilo,” alisema Mbwilo.

Alisema kutokana na umoja huo wachimbaji wataweza kuungana kwa pamoja na kuwezesha bei ya milipuko kushuka na pia kupatikana kwa wasambazaji wengi wa zana za milipuko hivyo kupatikana kwa urahisi.

Naye,Kamishna msaidizi wa madini kanda ya kaskazini,Benjamin Mchwampaka alisema eneo tengefu la Mirerani lilianzishwa mwaka 2003 baada ya Waziri wa nishati na madini kushauriana na mkuu wa mkoa huo juu ya uanzishwaji wake.

Mhandisi Mchwampaka alisema kuwa katika eneo la Tanzanite kuna makampuni makubwa manne yanayochimba kwenye eneo hilo na wachimbaji wadogo idadi yao ni 500 wanaomiliki migodi kwenye vitalu B na D.

Alisema ofisi yake kupitia wataalamu mbalimbali wakiwemo waandisi na wajiolojia wanashirikiana na wachimbaji wakubwa,wakati na wadogo katika kufanikisha shughuli za uchimbaji wa madini ya Tanzanite.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post