Jumuiaya ya Afrika Mashariki (EAC) itafanya mjadala wa kisiasa kwa mara ya kwanza kati ya Novemba 17 na 18, mwaka huu mjini Kampala, Uganda kwa lengo la kutangaza na kuwajulisha wananchi wa kanda hiyo juu ya hatua iliyofikiwa ya ushirikiano wa kisiasa, kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu wa EAC, anayeshughulikia Shirikisho la Kisiasa, Beatrice Kiraso.
‘’Mjadala huo unalenga kukuza taratibu za ushirikiano na uwakilishi katika mchakato mzima pamoja na mguso wa siasa za kitaifa katika ushirikiano wa kanda,’’chanzo cha habari toka ndani ya EAC, Libeneke la kaskazini
Wajumbe wapatao 50 wakiwemo wataalamu, vijana, wasomi,mashirika ya dini, waandishi wa habari na wanasiasa wanatarajiwa kushiriki katika mjadala huo.
Changamoto katika ushirikiano wa kisiasa
Kwa kuzingatia tafiti zilizofanywa awali na mashauriano, raia wengi wa Afrika Mashariki wanaogopa kwamba utawala mbovu, ikiwa ni pamoja na rushwa, ukiukwaji wa haki za binadamu na kushidwa kuheshimu katiba na utawala wa sheria, kama havitashughulikiwa ipasavyo, upo uwezekano wa kuhamia kwenye nchi wananchama, umetahadharisha waraka uliopelekwa kwa washiriki.
Kwa maoni yao, ushirikiano wa kisiasa unaweza kurudisha nyuma maendeleo yaliyofikiwa kitaifa kwa mfano, katika kubadilishana uongozi kwa amani au mapambano dhidi ya rushwa. Kumekuwepo pia na wasiwasi kwamba kukosekana kwa demokrasia na uwajibikaji uliopo katika baadhi ya nchi wananchama, unaweza kuambukiza kanda nzima ikiwa ni pamoja na tofauti za mifumo ya kisisa.
Umuhimu wa mjadala Kwa kuzingatia falsafa ya ushirikiano wenye msingi toka kwa wananchi wenyewe, ni muhimu kuwashirikisha wadau wote kwa namna ya kuleta manufaa ya kweli. Mjadala huo ni moja ya juhudi za EAC katika kuelekea kwenye mdahalo mkuu wa mtangamano wa kisiasa.
Kwa mujibu wa Naibu Katibu Mkuu wa EAC, Kiraso, mjadala wa aiana hiyo utakuwa unafanyika mara kwa mara katika nchi wananchama kwa kuzingatia tafiti zinazofanywa kwa maelekezo ya sekretarieti ya EAC.