MGODI wa mchimbaji mdogo wa madini ya Tanzanite wa mji mdogo wa Mirerani,wilayani Simanjiro,mkoani Manyara,unaomilikiwa na Deo Minja umelipuka moto na kuteketeza mali zenye thamani ya mamilioni.
Katika tukio hilo,kulitokea mlipuko mkubwa mithili ya bomu hali iliyosababisha hofu miongoni mwa wachimbaji wa madini wa madini ya Tanzanite na wakazi wa mji mdogo wa Mirerani pamoja na viunga vyake.
Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi mkoani Manyara,Kamishna msaidizi Liberatus Sabas,tukio hilo lilitokea juzi mwaka huu saa 5 usiku,kwenye mgodi huo uliopo katika eneo la kitalu B (Opec) mji mdogo wa Mirerani wilayani humo.
Kamanda Sabas alisema kuwa katika tukio hilo hakuna mtu yeyote aliyejeruhiwa au aliyefariki dunia,zaidi ya mali zenye thamani za mamilioni ya shilingi kuteketea kwa moto ikiwemo mashine za kuendesha mgodi huo.
Alisema jeshi lake linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo,ili kubaini chanzo cha tukio hilo na kujua thamani halisi ya mali zilizoteketezwa kwenye tukio hilo la kutokea kwa moto na mlipuko mgodini hapo.
Akizungumza mara baada ya tukio hilo,mmiliki wa mgodi huo Deo Minja,alisema wakati moto huo ukitokea hakukuwa na nishati ya umeme kwani walikatiwa kutokana na deni walilokuwa wanadaiwa na Tanesko.
Minja alisema walikuwa wanadaiwa na Tanesko zaidi ya sh2 milioni na walilipa kianzio cha sh1.5 milioni,ili warudishiwe umeme huo lakini mlipuko huo ulitokea usiku kabla umeme haujarudishwa kwenye mgodi wake.
“Tunamshukuru Mungu,kwani kwenye tukio hilo hakukuwa na mtu yeyote aliyejeruhiwa au kufariki dunia,ambapo wafanyakazi wa mgodi walikuwa wamejipumzisha kutokana na kutokuwepo kwa umeme,” alisema Minja.
Kwa upande wake,Kamishna msaidizi wa madini kanda ya kaskazini,Mhandisi Benjamin Mchwampaka,amewataka wachimbaji wadogo wa madini ya Tanzanite kuchukua tahadhari pindi wanapoendesha shughuli zao migodini.
Mchwampaka alisema wachimbaji wadogo wanapokuwa wanafanya shughuli za mgodini kwa uangalifu,wataepusha mambo mengi ikiwemo ajali zinazoweza kuepukika hivyo kutoathiri shughuli zao za kila siku.
Hata hivyo,baadhi ya wachimbaji wa mgodini huo walidai kuwa,moto na mlipuko huo,ulisababishwa na mmoja wapo kati ya watunza zana za milipuko anayedaiwa kuiba zana kadhaa na kulipua nyingine ili kuondoa ushahidi.
“Huo ulikuwa mpango wa mtu na lengo lake ilikuwa azichome zana chache ili apoteze ushahidi baada ya kuchukua baadhi ya zana na kuziuza ili ajipatie fedha kidogo lakini hakutegemea kama hasara kubwa kiasi hicho ingetokea,” walisema.