Wadau
mbalimbali wa madini ya vito waliopata bahati kutembelea Banda la
Tanzania katika siku ya kwanza ya Maonesho ya 54 ya Kimataifa ya Vito na
Usonara ya Bangkok, wakishangazwa na mng’ao wa Kito cha Tanzanite
katika Pete iliyovalishwa kidoleni mwa Mwanafunzi, Raia wa Thailand
aliyeomba kujaribisha Pete hiyo. Anayetoa maelezo ni Mfanyabiashara wa
Madini ya Vito kutoka Tanzania, Bw. Gregory Kibusi (Mwenye mavazi ya
Bhatiki).
Mkurugenzi
wa Kitengo cha Uthaminishaji wa Madini ya Almasi na Vito cha Wizara ya
Nishati na Madini (TANSORT), Archard Kalugendo akizungumza na mdau wa
madini ya vito aliyetembelea Banda la Tanzania. Kalugendo alitumia fursa
hiyo kumkaribisha mdau huyo katika Maonesho ya Vito ya Arusha
yanayotarajiwa kufanyika mwezi Septemba mwaka huu nchini Tanzania.
Katikati ni Afisa kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Asimwe Kafrika.
Sehemu
ya shehena ya madini mbalimbali ya vito katika Banda la Tanzania kwenye
Maonesho ya 54 ya Kimataifa ya Vito na Usonara ya Bangkok.
Wafanyabiashara
wa Madini ya Vito kutoka Tanzania, Gregory Kibusi (Mwenye nguo za
Bhatiki) na Kassim Iddi Pazi (Mwenye Shati la rangi ya Bluu),
wakimwonyesha Mteja aina mbalimbali za madini ya vito yanayopatikana
Tanzania.
Mgeni
Rasmi katika ufunguzi wa Maonesho ya 54 ya Kimataifa ya Vito na Usonara
ya Bangkok, ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara ya Thailand, Bi.
Chutima Bunyapraphasara, akikata utepe kuzindua rasmi Maonesho hayo.
Kushoto kwake ni Rais wa Taasisi ya Wafanyabiashara wa Madini ya Vito wa
Thailand, Bw. Somchai Phornchindarak na Kulia kwake ni Mkurugenzi
Mtendaji wa Idara ya Uhamasishaji Biashara Kimataifa, Bibi Nuntawan
Sakuntanaga.
Baadhi
ya Viongozi kutoka Taasisi na Mashirika mbalimbali ya kiserikali na
binafsi yanayoshiriki katika Maonesho ya 54 ya Kimataifa ya Vito na
Usonara ya Bangkok, wakiwa katika picha ya pamoja na Mgeni Rasmi, Katibu
Mkuu wa Wizara ya Biashara ya Thailand, Bi. Chutima Bunyapraphasara
(katikati – mwenye sketi ndefu).
Mkurugenzi
wa Kitengo cha Uthaminishaji wa Madini ya Almasi na Vito cha Wizara ya
Nishati na Madini - Tanzania (TANSORT), Archard Kalugendo (wa kwanza
kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na Kamati iliyoandaa maonesho
husika.
Mkurugenzi
wa Kitengo cha Uthaminishaji wa Madini ya Almasi na Vito cha Wizara ya
Nishati na Madini - Tanzania (TANSORT), Archard Kalugendo akisalimiana
na Rais wa Taasisi ya Wafanyabiashara wa Madini ya Vito wa Thailand, Bw.
Somchai Phornchindarak baada ya uzinduzi rasmi wa maonesho hayo.
Na Veronica Simba - Bangkok
Banda
la Tanzania katika siku ya kwanza ya Maonesho ya 54 ya Kimataifa ya Vito
na Usonara ya Bangkok, yaliyozinduliwa Septemba 9, 2014 nchini
Thailand, limekuwa na mvuto wa kipekee kwa wadau wa madini husika kutoka
mataifa mbalimbali duniani waliofika katika maonesho hayo.
Mkuu
wa Banda la Tanzania, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Kitengo cha
Uthaminishaji wa Madini ya Almasi na Vito cha Wizara ya Nishati na
Madini (TANSORT), Archard Kalugendo alisema, wadau wengi waliofika
katika maonesho hayo, walivutwa na aina mbalimbali za madini ya vito
yanayopatikana Tanzania hususan Tanzanite.
“Unajua,
Tanzanite ni madini yanayopatikana Tanzania pekee ambapo sifa hii
inayafanya kuwa madini yenye mvuto wa pekee,” alisema Kalugendo.
Aliongeza kuwa, mbali na kuwa Tanzanite inapatikana Tanzania pekee,
lakini pia ina mvuto wa pekee machoni mwa watazamaji ambayo ni sababu
nyingine inayowavutia watu wengi kupenda kufahamu zaidi kuhusu madini
hayo, hali ambayo imesababisha watu wengi kutembelea Banda la Tanzania.
Alifafanua
kuwa, pamoja na kuwepo mabanda kutoka nchi nyingine yaliyo na madini ya
Tanzanite katika maonesho hayo, wengi wa wadau walitembelea Banda la
Tanzania wakitaka kuelimishwa zaidi kuhusu madini hayo, hali
inayodhihirisha kuwa ufahamu kwamba Tanzanite inatoka Tanzania pekee
umeongezeka kwa watu kutoka mataifa mbalimbali.
Wakizungumza
kwa nyakati tofauti, Wafanyabiashara wa Madini ya Vito kutoka Tanzania
wanaoshiriki katika maonesho hayo, Gregory Kibusi na Kassim Pazi
walisema ushiriki wa Tanzania katika maonesho husika kwa msimu huu
umeboreka zaidi kutokana na maandalizi mazuri yaliyofanyika.
“Tulitumia
uzoefu tulioupata katika maonesho ya msimu uliopita na hivyo
tukajipanga vizuri zaidi kuhakikisha tunakuwa na ushiriki wenye tija
msimu huu na ndiyo maana katika siku ya kwanza tu ya maonesho,
tumeshuhudia banda letu likitembelewa na watu wengi sana,” alisema
Kibusi.
Naye
Gregory alifafanua kuwa maandalizi waliyofanya ni pamoja na kuandaa
madini ya kutosha hasa yale yaliyokatwa tayari, ambayo ndiyo
yanayopendwa zaidi na wadau wengi wanaofika katika maonesho.
Kwa
upande wake, Mtaalamu wa Madini ya Vito kutoka TANSORT, ambao ndiyo
waratibu na wasimamizi wa ushiriki wa Tanzania katika maonesho hayo,
Teddy Goliama alisema maandalizi mengine yaliyofanyika ni pamoja na
kuwepo na washiriki wengi zaidi wakijumuisha wachimbaji na
wafanyabiashara wa madini husika pamoja na maafisa kutoka Wizarani.
Vilevile
alisema kuwa, mbali na kutangaza madini mbalimbali yaliyopo Tanzania,
Ujumbe wa Tanzania unaoshiriki katika maonesho hayo unafanya kazi ya
kuitangaza nchi kwa ujumla ikiwa ni pamoja na fursa mbalimbali za
uwekezaji pamoja na vivutio vya utalii.
“Tumeamua
kutumia fursa hii ya maonesho kuitangaza nchi kwa ujumla. Tunawashukuru
Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Bodi ya Utalii ambao walitupatia
vipeperushi, picha za video na makabrasha mbalimbali yenye kutangaza
vivutio vya utalii wa nchi yetu. Tumegawa vipeperushi vingi ambavyo
tunaamini vitasaidia sana kuitangaza nchi yetu katika anga za kimataifa
na hivyo kuvutia watalii na wawekezaji wengi zaidi,” alisema Teddy.
Maonesho
ya 54 ya Kimataifa ya Vito na Usonara ya Bangkok, yaliyofunguliwa
Septemba 9 mwaka huu na Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara ya Thailand,
Bi. Chutima Bunyapraphasara, yanatarajiwa kuhitimishwa Septemba 13,
2014. Hii ni mara ya pili kwa Tanzania kushiriki maonesho hayo.