Mfugaji Gwarudaa Lele mwenye ng’ombe
1,800 amepewa siku 10 na wana kijiji wa Oltukai, Kata ya Esilalei, Wilayani
Monduli Mkoani Arusha, kuondoka na mifugo yake kijijini hapo akidaiwa kuishi
bila kuwa na kibali.
Wakizungumza na waandishi wa habari
juzi, wana kijiji hao walidai kuwa Lele alipewa hifadhi ya muda kwenye kijiji
hicho ila akanogewa na kutaka kuendelea kuishi katika kijiji chao ili hali
hajapata ridhaa ya wananchi hao.
Mkazi wa kijiji hicho, Lazaro Mabengo akizungumza
huku akiwa na jazba alisema Lele alifika
eneo hilo na kuomba sehemu ya kujihifadhi akiwa na ng’ombe 200 lakini
ameng’ang’ania hadi kufikisha ng’ombe 1,800.
“Huyu mtu amekuwa chanzo cha migogoro na
kero kubwa kwenye kijiji chetu, pia mifugo yetu imekosa malisho kutokana na
yeye kuwa na mifugo mingi inayoleta matatizo kwa wafugaji wa kijiji hiki,”
alisema Mabengo.
Kwa upande wake diwani wa kata ya
Esilalei, Malunga Nangari alisema Lele alivamia eneo la mkazi wa kijiji hicho
Lelukunya Kirina, lenye ukubwa wa ekari tatu lililopo karibu na eneo la umma
lililotengwa kwa ajili ya malisho.
Nangari alisema mfugaji huyo anatakiwa
kuondoka eneo hilo kwani hana kibali chochote kinachomruhusu kuishi hapo,
kutokana na kuwa awali aliomba kuishi kwa muda mfupi kipindi cha ukame ila
akanogewa na kukaa hadi sasa.
Hata hivyo, Lele akizungumza na
waandishi wa habari alisema wivu, chuki na ubaguzi wa baadhi ya wakazi wa eneo
hilo, ndiyo umesababisha afukuzwe kwenye kijiji hicho japo aliishi vizuri na
kufuata taratibu zote za eneo hilo.
“Huu ni ubaguzi jamani sasa kama siyo
mauaji ni nini, kwa sababu mimi ni mang’ati ndiyo wananifanyia hivi karibu
kijiji kizima nilishawapa ng’ombe zangu lakini nashangaa leo wananifukuza mimi
siondoki, niende wapi?” alihoji Lele.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia