Vikundi vya wakulima 920 wa zao la ufuta
wa Tarafa ya Mbugwe Wilaya ya Babati Mkoa wa Manyara, wamefaidika kiuchumi
baada ya kuwezeshwa na shirika la Farm Africa, kwa kufanya kuwa zao tegemezi
kwenye biashara.
Akizungumza juzi kwenye warsha ya wadau
wa ufuta iliyofanyika wilayani Babati, Mratibu wa mradi wa ufuta wa Farm
Africa, William Mwakyami alisema kati ya wakulima hao 920 wanaume ni 490 na
wanawake ni 430.
Mwakyami alisema wakati awamu ya pili ya
mradi wa ufuta ikitarajia kufikia mwishoni mwezi Octoba mwaka huu, kupitia Farm
Africa wameweza kuongeza kipato cha kaya kwa asilimia 20 na kuwaunganisha
wakulima na masoko.
Hata hivyo, alisema japokuwa ufuta
kutoka Tanzania una soko kubwa duniani kuliko nchi nyingine za bara la Afrika,
lakini haulimwi kwa wingi kwani nchi ya Sudan ndiyo inayoongoza kwa kuzalisha
kwa wingi zao la ufuta.
“Ufuta wetu ndiyo unaoongoza kwa ubora
kuliko ufuta kutoka nchi nyingine hivyo tunatakiwa tujitahidi kulima zaidi
kwani wenzetu Sudan japokuwa sehemu kubwa ni jangwa lakini wanalima ufuta
mwingi,” alisema Mwakyami.
Naye, Ofisa kilimo wa Farm Africa,
Tumaini Elibariki alisema miongoni mwa mafanikio ya wakulima hao ni kuongezaka
kwa uzalishaji wa mbegu bora ya ufuta kutoka kilo 2,000 (tani 2) hadi
kilo 11,180 (tani 11.18).
“Kilimo hiki kimesababisha kuongezeka
kwa kipato kwa wakulima hao kutokana na uzalishaji wa ufuta kutoka sh728,669 hadi kufikia sh2 milioni na mawakala
10 wamewaelimisha wakulima wengi kutumia pembejeo za kilimo,” alisema
Elibariki.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia