Madereva wa magari na pikipiki wa
Tarafa ya Sunya Wilayani Kiteto Mkoani Manyara, wamepatiwa mafunzo ya kuendesha
vyombo hivyo vya moto kwa lengo la kutokomeza ajali za uzembe zinazotokea kila
wakati hapa nchini.
Akizungumza baada ya kumalizika kwa
mafunzo hayo juzi, Ofisa wa polisi jamii Tarafa ya Sunya, Inspekta Said Alute alisema
madereva waliohitimu ni kutoka Kata za
Sunya na Dongo na walifundishwa na wataalam kutoka taasisi ya Apex.
Inspekta Alute alitoa wito kwa washiriki
wote waliohitimu mafunzo hayo ya udereva kutekeleza kwa vitendo yale yote
waliyofundishwa na walimu, hivyo wakakate leseni baada ya kulipia fedha zao mamlaka
ya mapato nchini (TRA).
“Kupitia Ofisa Tarafa ya Sunya,
watendaji wa kata za Dongo na Sunya, wenyeviti, watendaji wa vijiji na wananchi
kwa ujumla, wakuchukulie mafunzo haya kama mwanga wa kupunguza ajali zisizo za
lazima zinazotokea,” alisema.
Alisema wahitimu hao wanatakiwa
kuheshimu na kufuata sheria za usalama barabarani hapa nchini kwani kupitia
mafunzo hayo watakuwa wamejengewa uwezo wa kutosha wa kuwa makini pindi wawapo
barabarani.
Kwa upande wao baadhi ya washiriki wa
mafunzo hayo walilishukuru jeshi la polisi na taasisi ya Apex kwa kuandaa
mafunzo hayo, kwani hivi sasa wataweza kupatiwa leseni za udereva na kuondokana
na usumbufu waliokuwa nao.
Mmoja kati ya washiriki wa mafunzo hayo
Hamis Juma alisema ajali zinazotokea kutokana na uzembe au zinazoepukika, hivi
sasa zitapungua kwenye Tarafa hiyo ya Sunya, kwani elimu hiyo itawanufaisha
ipasavyo endapo ikitumika vizuri.