POLISI WAPIGWA BOMU

Jeshi la Polisi limeendelea kukumbwa na majanga kufuatia askari wake wawili kushambuliwa kwa mlipuko unaodhaniwa kuwa ni bomu mkoani Ruvuma.

Askari hao wa Kituo cha Polisi Mkoa wa Ruvuma, Konstebo Ramadhani Ally na WP Felista Makala,wamejeruhiwa baada ya kupigwa na kitu kinachosadikiwa kuwa ni bomu juzi usiku katika  mtaa wa Mabatini kata ya Misufini, karibu na nyumba ya wageni wakati  wakiwa katika doria.


Habari zilizopatikana jana mjini hapa kuthibitishwa na Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Ignas Nchimbi, zinasema kuwa tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa 1.30 usiku.


Kwa mujibu wa habari hizo, askari wanne wakiwa kwenye doria, walisikia kishindo kikubwa.


Nchimbi alisema akiwa nyumbani kwake akiendelea kufanya shughuli zake za kawaida, alisikia mlio mkubwa unaohofiwa kuwa ni bomu.Alisema baada ya kusikia hivyo, alitoka nje na kwamba, watu wengine waliokuwa katika eneo hilo, waliingiwa na hofu na kujifungia majumbani mwao.


Nchimbi, alisema baada ya muda alikwenda kwenye eneo la tukio na kukuta masalia ya misumari, vipande vya bati na chupa ya plastiki, vinavyosadikiwa kutumika kulipua bomu hilo.


Alisema aliwasiliana na uongozi wa serikali ya kata kabla ya taarifa za tukio hilo kutolewa polisi.


Nchimbi alisema baadhi ya nyumba zilizokuwa jirani na eneo la tukio zimeathirika, ikiwamo kuvunjika vioo vya madirisha na nyingine kupata nyufa.


Aliwataja wamiliki wa nyumba zilizoathirika kuwa ni Charles Lipochi, ambaye baadhi ya masalia yanayosadikiwa kuwa ni ya bomu yamekutwa kwenye eneo la nyumba yake.


Mwingine ni Akwinata Nombo, ambaye ni mmiliki wa nyumba hiyo  ya wageni iliyoharibiwa vioo vya madirisha na kupatwa na nyufa kwenye kuta na nyingine ni iliyokuwa ya marehemu Mathias Bula, ambayo nayo imeharibiwa vioo.


Ofisa Mtendaji wa Mtaa huo, Saada Mlowe, alisema idadi kubwa ya wananchi wanaoishi kwenye mtaa wake, bado wanasumbuliwa na hofu tangu kutokea tukio hilo litokee.


Lakini akalishukuru jeshi hilo kwa kuimarisha ulinzi kwenye eneo la tukio hadi sasa.Ofisa Tarafa ya Mashariki, Barnabas Ruhumbi, alisema ofisi yake imepata taarifa ya tukio hilo na kwamba, kwa sasa wanatarajia kukutana na mabalozi wote wa nyumba kumi pamoja na wenyeviti wa serikali za mitaa kuzungumzia kwa undani tukio hilo ili kuweka tahadhari.


RC: NI TUKIO LA KIHALIFU

Mkuu wa Mkoa huo, Said Mwambungu, alisema tukio hilo ni la kihalifu na kwa hiyo, serikali inafanya kila iwezekanavyo kuwasaka na kuwatia mbaroni wahusika ili sheria ichukue mkondo wake.

Aliwaomba wananchi kuwa watulivu na wavumilivu katika kipindi hiki, ambacho vyombo vya dola vinaendelea na uchunguzi.


MGANGA WA MKOA ANENA

Mganga Mkuu wa Mkoa huo, Dk. Daniel Malekela, alithibitisha kupokea majeruhi wawili, ambao wamelazwa kwenye Hospitali ya Mkoa Songea (Homso) na kwamba, waneendelea kupata matibabu.

Alisema watu hao wamejeruhiwa miguuni na kwamba, wanatakiwa kufanyiwa upasuaji mkubwa ili kuondoa vipande vya vyuma, ambavyo vipo ndani ya miguu yao.


KAULI YA POLISI

Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, George Chiposi, pamoja na kuthibitisha kutokea kwa tukio hilo, alisema taarifa zaidi zitatolewa na mamlaka ya juu ya jeshi hilo.

Hata hivyo, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Advera Senso, alipoulizwa na NIPASHE jana alithibitisha kuwapo kwa tukio hilo.


Alisema Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Isaya Mngulu, amekwenda kwenye eneo la tukio akiongozana na jopo la wataalamu wa masuala ya mabomu kwa ajili ya uchunguzi wa kina.


TUKIO LA KARIBUNI

Tukio hilo limetokea wiki moja baada ya askari wawili kuuawa na bunduki 10 aina ya SMG kuporwa katika Kituo  cha Polisi wilayani Bukombe mkoa wa Geita, Septemba 9, mwaka huu.

Uporaji huo ulifanywa na watu, ambao hawajafahamika baada ya kuvamia kituo hicho saa 9:45 alfajiri na kuwashambulia askari polisi waliokuwa zamu, wawili waliuawa na wengine watatu kujeruhiwa.


Mbali na kupora SMG 10, pia walipora risasi, ambazo idadi yake haijafahamika, pamoja na mabomu ya kutupa kwa mkono, ambayo walitokomea nayo kusikojulikana.


Kutokana na tukio hilo, Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, alilazimika kwenda Bukombe jana akiwa ameambatana na Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Geita, ikiongozwa na mwenyekiti wake, Mkuu wa Mkoa, Saidi Magalula.

About Woinde Shizza

Mwandishi , Mjasiriamali na Mbunifu wa Mavazi. Email : woindeshizza@gmail.com , Instagram: woindeshizzablog.