Ticker

6/recent/ticker-posts

ARUMERU HAPATOSHI WANANCHI WACHARUKA WABOMOA NYUMBA NA KUFYEKA MAZAO KWENYE VYANZO VYA MAJI

Vijana wakiwa na mabango kupinga uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji.

Upandaji miti kwaajili ya utunzaji wa mazingira

Ubomoaji wa nyumba ukiendelea

Wananchi wakikagua chanzo kilichogeuzwa shamba

Arumeru.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida wananchi wa Kata ya Ngarenanyuki,wilayani Arumeru,wamebomoa nyumba moja iliyojengwa kwenye chanzo cha maji  ili kunusuru vyanzo hivyo ambavyo viko hatarini kukauka kutokana na ujenzi usiozingatia utunzaji wa mazingira.
 
Wananchi waliotekeleza hatua hiyo,Steven John na Frank Nnko walisema kuwa  wamechukua uamuzi huo baada ya serikali kushindwa kuwachukulia hatua za kisheria watuhumiwa wa uvamizi wa vyanzo vya maji .
 
Nnko alisema mgogoro huo umedumu kwa muda mrefu kutokana na kuwa wananchi ndio waathirika wakubwa wa kukauka kwa vyanzo vya maji na kwamba  wameamua kujichukulia sheria mkononi na hawatasita kufanya hivyo kwa wananchi wengine watakaokiuka utunzaji wa mazingira.
 
Alifafanua kuwa kitongoji cha Momela ndicho chanzo kikuu cha maji katika Kata za King'ori,Makiba na Ngarenanyuki hivyo kuendelea kuwaachia wananchi wachache kuharibu mazingira kunaweza kugeuza eneo lote jangwa jambo ambalo linaweza kuhatarisha uhai wa watu na viumbe hai.
 
Mwenyekiti wa  jumuiya ya Maji bonde dogo  la Ngarenanyuki  ,Aminieli Mungure alisema kuwa  vyanzo hivyo vimekua vikiharibiwa kwa  kukosa usimamizi hivyo wakati umefika wa jamii kuamka na kuvilinda kwaajili ya kizazi cha sasa na kijacho.
 
Aliongeza kuwa Bonde dogo la Ngarenanyuki linahudumia vijiji  vinne ambavyo ni Ngabobo, Olkung’wado,Uvizo na Ngarenanyuki na kuwa wataanza kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kutunza mazingira pamoja na vyanzo vya maji.

Post a Comment

0 Comments