MBRAZIL
Marcio Maximo amepoteza mechi yake ya kwanza akiiongoza Yanga baada ya
kukubali kipigo ‘swaafi’ kabisa cha mabao 2-0 kutoka kwa Mtibwa Sugar,
uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro jioni hii.
Katika
mechi hiyo ya kukata na shoka, Mbrazil mwingine, Geilson Santos Santana
‘Jaja’ naye ameweka rekodi ya kukosa mkwaju wa kwanza wa penalti
akiichezea Yanga katika mechi yake ya kwanza ya ligi kuu.
Mabingwa
hao wa 1999 na 2000 wakiongozwa na mwanafunzi wa zamani wa Maximo,
Mecky Mexime, waliandika bao la kuongoza katika dakika ya 15 kipindi cha
kwanza kupitia kwa mshambuliaji wao hatari, Musa Hassan Mgossi.
Nahodha
wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alifanya makosa ya kumsindikiza
Mgosi katika eneo la hatari akiamini kipa Deogratius Munishi ‘Dida’
ataokoa, lakini hakufanikiwa na kumpa nafasi nyota huyo wa zamani wa
Simba kuandika bao kimiani .
Yondan
alishindwa kuosha mpira mrefu wa juu kwa kichwa na kuangukia eneo
ambalo si mabeki wala kipa ambaye angeweza kuokoa kiurahisi. Licha ya
Oscar Joshua kuingia kusaidia kuokoa, Mgosi alimchengua Dida aliyetoka
langoni mwake na kufungwa goli hilo.
Wakati
wachezaji wa Mtibwa wakishangilia bao hilo, nyuki walipita uwanjani
hapo na kusababisha baadhi ya wachezaji wa timu zote kulala chini ili
kukwepa madhara.
Dakika
ya 32 Jaja almanusura aandike bao safi kwa kichwa akiunganisha kona
iliyopigwa na Haruna Niyonzima, lakini mabeki wa Mtibwa waliondoa mpira
katika mstari wa golini na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Kwa
ujumla dakika 45 za kipindi cha kwanza sola lilianza kwa presha kubwa,
na kushuhudia timu zote zikicheza mpira wa ‘butu-butu’.
Hata hivyo, Yanga walionekana kufika mara nyingine golini na kupiga mashuti 5 yaliyolenga goli wakati Mtibwa walipiga 2 tu.
Yanga
walionekana kutofanya vizuri sehemu ya kiungo mpaka pale kocha Marcio
Maximo alipoamua kumtoa Oscar Joshua na kumuingiza Omega Seme.
Mabadiliko
hayo yalimlazimisha Mbuyu Twite arudi sehemu ya ulinzi wa kushoto na
kumpisha Seme sehemu ya kiungo. Mabadiliko hayo yaliwapa nguvu Yanga na
kutawala sehemu ya kiungo.
Hata
hivyo licha ya kutawala sehemu ya kati na kumiliki mpira kwa asilimia
52 kwa 48 katika kipindi hicho cha kwanza, Yanga walikosa mipango
sehemu ya mwisho na kukosa nafasi za kufunga.
Sehemu
ya ulinzi ya Yanga haikucheza vizuri katika dakika za kipindi cha
kwanza na hii ilichangiwa na sehemu ya kiungo kushindwa kufanya kazi
yake vizuri.
Haruna
Niyonzima na Hassan Dilunga hawakuonekana kucheza mpira wao uliozoeleka
na walitawaliwa na viungo wa Mtibwa akiwemo Mkongwe Shaban Nditi.
Kutokana
na Yanga kufa sehemu ya kiungo, Cannavaro na Yondani walishindwa
kutimiza majukumu yao na mara kadhaa kulitokea presha kubwa langoni
mwao.
Yondani alionekana kukosa utulivu na kufanya baadhi ya faulo ambazo kwa bahati nzuri mwamuzi hakuziona.
Kipindi
cha pili, Yanga walianza mpira kwa kasi wakishambulia kutoka upande wa
kulia ambako Mrisho Ngassa alionekana kuwa hatari zaidi.
Dakika
ya 45 Ngassa alipiga krosi kutoka winga hiyo ya kulia na ukagonga
katika mkono wa nahodha wa Mtibwa, Nditi na mpira kumpata Jaja aliyetia
nyavuni, lakini mwamuzi alikataa goli hilo na badala yake kutoa penalti.
Jaja
katika dakika 46 alipewa penalti yake ya kwanza akiichezea Yanga,
lakini alikosa baada ya kipa Said Mohamed kuokoa kwa mguu wake wa
kushoto.
Dakika
moja baadaye, Yanga walishambulia kwa kasi na Saimon Msuva aliyeingia
kuchukua nafasi ya Hamis Kiiza alitia nyavuni mpira, lakini mwamuzi
msaidizi alikataa bao hilo akidai winga huyo aliotea.
Dakika
ya 51 Niyonzima alipiga mpira wa adhabu ndogo na kuunganishwa kwa njia
ya kichwa na Cannavaro, lakini ‘Mchawi’ wa Yanga leo hii, Kipa Mohamed
aliudaka mpira huo.
Dakika
ya 61, Niyonzima alipiga mpira mwingine wa adhabu ndogo uliotua
kichwani kwa Jaja , lakini kipa aliokoa kwa mara nyingine.
Jaja
aliyepata mipira minne mizuri, alitia kambani mmoja lakini goli
lilikataliwa na mitatu alipiga vichwa vya hatari. Hii inaonesha
mshambuliaji huyo kutoka Brazil ni mtu wa kuchungwa.
Dakika ya 69, Msuva alienda golini kwa Mtibwa na kutoa mfuko wa ‘Gloves’ za kipa Said Mohamed ingawa haikujulikani ni kwanini.
Kwa
tamaduni za soka la Tanzania, inawezekana Msuva amehisi mfuko ule ndio
unawazuia kufunga magoli. Kifupi ni kama imani za kishirikina.
Dakika
ya 82 Amel Ally alipata mpira mrefu na kusumbuana na Cannavaro akiwa na
mwenzake Yondani, akatishia akapiga mpira wa juu ambapo kipa Dida
alipaa juu na kujaribu kuokoa, lakini ukazama nyavuni na kuiandikia
Mtibwa bao la pili.
Goli
hilo lilitokana na uzembe wa mabeki wa Yanga ambapo kwa muda mrefu timu
yao ilikuwa ikishambulia na mpira ulipopigwa hawakuwa tayari
kukuabiliana na shambulizi hilo la kushitukiza
Kwa ujumla kipindi cha pili Yanga walitawala mpira na kufika langoni kwa Mtibwa mara nyingi zaidi, lakini mambo yalikuwa magumu.
Katika
kipindi hicho, Yanga walimiliki mpira kwa asilimia 54 kwa 46, lakini
haikuwasaidia kukwepa kipigo hicho kutoka kwa wakata miwa wa Manungu
Turiani
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia