MANISPAA YA ILEMELA YAANZA BOMOA BOMOA KWA WALIOJENGA KWENYE HIFADHI YA MTO MSUKA KILIMAHEWA.

Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza imeanza utekelezaji wa zoezi la kubomoa kuta za nyumba zilizojengwa kwenye hifadhi ya Mto Msuka katika eneo la Kilimahewa, kwa ajili ya kupanua mto huo ili kuondoa athari za mafuriko zinazojitokeza wakati wa mvua za masika. Wananchi wametakiwa kutojenga maeneo yasiyo rasmi.
Na BMG
Zoezi ka ubomoaji likiendelewa ambapo limesimamiwa na mgambo wa halmashauri hiyo ya Manispaa ya Ilemela
Mto huu unapaswa kupanuliwa zaidi na kujengewa kuta maana wakati wa mafuriko huwa unapitisha maji mengi yanayosababisha mafuriko kwa wakazi wa eneo hili la Kilimahewa.
Miongoni mwa kuta zilizoingia eneo la hifadhi ya mto Msuka baada ya kubobolewa
Miongoni mwa kuta zilizoingia eneo la hifadhi ya mto Msuka baada ya kubobolewa
Na George Binagi-GB Pazzo 
Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza imeanza utekelezaji wa zoezi la kubomoa kuta za nyumba zilizojengwa kwenye hifadhi ya Mto Msuka katika eneo la Kilimahewa, kwa ajili ya kupanua mto huo ili kuondoa athari za mafuriko zinazojitokeza wakati wa mvua za masika.

Mhandisi wa Manispaa hiyo, Jacob Mwakyambiki, amesema zoezi hilo limefanyika baada ya tahadhari kutolewa kwa wakazi wa eneo hilo kwa kipindi cha zaidi ya miezi sita na kwamba mpango uliopo ni kujenga mtaro mkubwa katika mto huo ili kusaidia maji yake kutosababisha mafuriko wakati wa mvua za masika.

Amesema tayari mkandarasi ameanza kazi hiyo na kwamba ujenzi wa mto huo utakapokamilika, utasaidia maji yake kutiririka moja kwa moja hadi ziwa Victoria badala ya kumwaga maji kwenye makazi ya watu kama ilivyokuwa hapo awali na kusababisha athari za kimafuriko.

Hata hivyo baadhi ya wakazi wanaoishi katika eneo linalopitiwa na mto Msuka wamesema zoezi hilo limefanyika wakati ambao bado hawajui hatima yao kwani wakati wanajenga makazi yao katika eneo hilo walipata vibali vyote ikiwemo hati miliki za viwanja vyao ambapo wamependekeza kulipwa fidia licha ya Manispaa ya Ilemela kuwatahadharisha kwamba hakuna fidia itakayotolewa kwa waliojenga katika hifadhi ya mto.

Licha ya malalamiko hayo, baadhi ya wakazi wa Kata ya Ibungilo wanaoishi katika maeneo jirani na mto Msuka wamepongeza zoezi la upanuzi wa mto huo kwani wamekuwa wakipata athari kubwa ikiwemo mali zao kusombwa na maji wakati wa mvua za masika kutokana na makazi ya wananchi yaliyojengwa kwenye karibu na mto huo.

Katika misimu kadhaa ya mvua za masika, athari mbalimbali ikiwemo vifo vya watu na mifugo kutokana na mafuriko ya mto Msuka, zimekuwa zikitokea katika eneo la Kilimahewa kutokana na wananchi kujenga makazi yao hadi kwenye hifadhi ya mto huo hivyo upanuzi na ujenzi wake unaelezwa kuwa mwarobaini wa kadhia hiyo.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post